
HUKU viongozi wakuu nchini wakituma risala za rambirambi kufuatia kifo cha Bw Chebukati, aliyekuwa mgombea wa urais wa muungano wa Azimio katika uchaguzi mkuu wa 2022 Raila Odinga na aliyekuwa mgombea mwenza wake Martha Karua walichelea kutuma jumbe zao.
Hata hivyo, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, ambaye angeteuliwa kuwa Waziri Mkuu, Odinga angeshinda, alituma ujumbe mfupi mistari miwili tu, kumwomboleza Bw Chebukati.
“Natuma rambirambi zangu kwa familia na marafiki wa aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati. Naiweka familia yake mawazoni na kwenye maombi wakati huu wa huzuni,” akasema kupitia akaunti yake ya mtandano wa kijamii wa X.
Kufikia sasa kumi jioni (4.00pm) Ijumaa, Februari 21, 2025, saa saba baada ya habari kuhusu kifo cha Bw Chebukati kutolewa rasmi, Bw Odinga hakuwa ametuma rambirambi zake wala kutuma ujumbe wa pole.
Uchunguzi wa Taifa Leo katika majukwa ya akaunti zake za mtandao ya kijamaa, anayotumia kila mara haswa kutuma risala za kuombeleza vifo vya watu mashuhuri, ulibaini kuwa ujumbe wake wa mwisho ni kuhusu mkutano kati yake na Rais wa Burundi Evareriste Ndayishimiye mnamo Februari 12, 2025.
Bw Odinga alikutana naye jijini Bunjumbura katika kampeni zake za mwisho za kuomba kura kuelekea uchaguzi wa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) ambapo alishindwa.
Kwa upande wake Bi Karua ujumbe wa mwisho kwenye akaunti yake ya X unahusu kujumuika kwake na raia wa kawaida wakifurahia kinywaji cha kahawa katika kibanda cha Sammy kituo cha kibiashara cha Githiga, eneo bunge la Gichugu, kaunti ya Kirinyaga.
Mnamo Agosti 15, 2022 marehemu Chebukati alimtangaza Rais William Ruto kama mshindi wa uchaguzi wa urais wa Agosti 9, matokeo yaliyopingwa na wawili hao kwa kuwasilisha kesi katika Mahakama ya Juu. Hata hivyo, kesi yao ilitupiliwa mbali na Dkt Ruto akaapishwa kuwa Rais wa tano wa Kenya.
Aliyekuwa naibu Rais Rigathi Gachagua pia alichelrea kumwomboleza Bw Chebukati.
Ujumbe wa mwisho katika akaunti yake ya X ni ule aliouweka Februari 14, 2025 kulaani hatua ya serikali ya Uganda kuendelea kumzuilia kiongozi wa upinzani Kizza Besigye anayekabiliwa na tuhuma za kuwa na silaha kinyume cha sheria.
Baadhi ya Wakenya kwenye mitandao ya kijamii alidai kuwa kifo ndio hatima inayowapata wenyeviti wa IEBC ambao kulingana nao hukutubali kutumiwa na wanasiasa kuendeleza wizi wa kura za urais.
“Wenyeviti wa IEBC wanaoongoza wizi wa kura huishia kufa kwa njia za kutatanisha., Kivuitu alikufa kutokana na kansa ya koo akiwa ametengwa kabisa. Wafula alikufa akiwa hajifamu,” anaeleza @Juma kupitia twitter.
Na Omosh anasema hivi: “Chebukati amekufa. Je, tunapaswa kusherehekea au kuhuzunika. Hamna mtu ambaye amewahi kukaidi matakwa ya raia ataishi kuona miaka mitano ijayo. Ilikuwa Kivuitu sasa ni Chebukati.”
Bw Samuel Kivuiti, ndiye alikuwa mwenyekiti wa ilikuwa Tume ya Uchaguzi Nchini (ECK) mnamo 2007. Ghasia zililipuka nchini baada yake kumtangaza Mwai Kibaki kama mshindi katika kinyang’anyiro cha urais mnamo Desemba 30, mwaka huu. Hii ni baada ya Bw Odinga na wafuasi wake kupinga matokeo ya uchaguzi huo.
Bw Kivuitu alikufa miaka miwili baadaye baada ya kuugua.
Leave a Reply