ALIYEKUWA Waziri Mkuu Raila Odinga atakabiliana na wapinzani wake katika wadhifa wa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) katika mdahalo wa televisheni utakaofanyika Desemba 13 kuwasilisha maono na mawazo yao ya kutekeleza Ajenda Afrika 2063.
Mjadala Afrika, ni mdahalo wa moja kwa moja unaotoa jukwaa kwa wagombeaji kuhutubia raia wa Afrika, kwa kuzingatia masuala ya sera na mwelekeo kuhusu jinsi kila mgombea ananuia kuendeleza matarajio na malengo ya Ajenda 2063.
Bw Odinga amesema kuwa yeye ndiye bora zaidi kwa Afrika, akisema anashawishika kwamba maono na anayopatia kipaumbele yataelekeza Afrika katika enzi mpya ya amani endelevu, ushirikiano wa bara, ustawi wa pamoja na ushirikiano.
Tume ilitangaza kuwa Mjadala Afrika utawapa wagombea wote fursa ya kutangaza mipango yao ya bara hili.
Mdahalo huo utakaofanyika katika makao makuu ya AU jijini Addis Ababa, Ethiopia utaendeshwa kwa Kifaransa na Kiingereza, huku tafsiri ikitolewa mbashara kwa wagombea na wasikilizaji katika lugha zote sita za muungano huo (Kiingereza, Kifaransa, Kiarabu, Kireno, Kihispania, na Kiswahili).
Leave a Reply