Raila na Ruto kugawana serikali siasa za 2027 zikichacha


SIASA za nchi zinatarajiwa kuchukua mkondo mwingine wiki ijayo wakati ambapo Rais William Ruto na Kinara wa Upinzani Raila Odinga wanatarajiwa kuweka wazi ushirikiano kati yao na kuunda serikali ya muungano.

Bw Odinga, Jumanne alianza ziara rasmi kwenye ngome zake za kisiasa ambapo alisema anashauriana na wafuasi wake kuhusu mwelekeo wa kisiasa ambao anastahili kuchukua kuelekea 2027.

Hata hivyo, duru kutoka kwa waliohudhuria mikutano ambayo aliandaa Kisumu, ngome yake ya kisiasa pamoja na Ikulu ya Mombasa zimearifu kuwa waziri huyo mkuu wa zamani ameshakata kauli kujiunga rasmi na utawala wa Rais Ruto.

Baadhi ya vijana ambao walihudhuria mkutano wa faragha na Raila Kisumu, walisema waziri huyo mkuu wa zamani aliwarai waunge mkono ushirikiano wake na Rais Ruto kwa sababu una manufaa kimaendeleo.

“Tulikuwa na mkutano na Baba ambapo alitutaka tujiandae kwa kuzinduliwa kwa ushirikiano wake na Rais Ruto wiki ijayo,” akasema kijana mmoja ambaye alihudhuria mkutano huo.

“Na iwapo kutakuwa na pingamizi, alitushauri tufafanulie wafuasi wake kwa nini ameamua kuchukua hatua hiyo muhimu akisema ni kwa sababu ya manufaa yao,” akaongeza.

Kulingana naye, Bw Odinga ameshaamua kuingia kwenye utawala wa Rais Ruto na yupo tayari kwa hali yoyote ile kuanza kazi ambayo itahakikisha baadhi ya sera za utawala zinazowaumiza Wakenya zinaondolewa.

Kabla ya kukutana na vijana hao, Bw Odinga pia aliandaa mkutano na wazee, washikadau na wanasiasa katika makazi yake kwenye milima ya Riat ambapo aliomba baraka zao kuhusu kuingia kwenye utawala wa Rais Ruto.

Wote hao walitoka kwenye ngome yake ya kisiasa ya kaunti za Migori, Kisumu, Homa Bay na Siaya. Bw Odinga pia alisema atakuwa akishauriana na wafuasi wake Bonde la Ufa, Pwani, Kaskazini Mashariki, Mashariki na Kati kuelekea tangazo kuu analotarajiwa kutoa wiki ijayo.

Waziri huyo mkuu wa zamani akifafanulia vijana hao sababu ya kuchukua hatua hiyo, alirejelea jinsi ambavyo Rais Ruto alisimama naye wakati wa kampeni ya uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) na kusema hawezi kumsaliti kamwe.

Kinara huyo wa ODM pia inasemekana alimshawishi Gavana wa Kisumu Profesa Anyang’ Nyongó ambaye alihudhuria mkutano huo, sababu zake za kujiunga na utawala wa Kenya Kwanza.

Profesa Nyong’o na Gavana wa Siaya James Orengo ni kati ya wandani wa Raila ambao wamekuwa mstari wa mbele kukosoa serikali ambapo baadhi ya wanachama wa ODM wanatumikia kama serikali.

Bw Orengo hakuwa kwenye mkutano ulioandaliwa Kisumu ila inasemekana Raila ameamua kumpiga kumbo kati ya wandani wake waaminifu.

Bw Odinga ameonekana kushaajishwa na wengi katika ngome zake kupinga ushirikiano wowote ambao anaweza kuwa nao na watu wa Mlima Kenya kupitia aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua. Ngome za Raila zilikerwa na wafuasi wa Bw Gachagua kumcheka alipokosa kiti cha AUC.

Seneta wa Siaya Dkt Oburu Oginga ambaye ni kake Raila ndiye duru zinaarifu alikuwa mhusika mkuu kuafikia mkataba wa kufanya kazi na Rais Ruto.

Ingawa yaliyomo kwenye mkataba huo hayajawekwa wazi, duru zinasema kuwa Rais anatarajiwa kufanya mabadiliko kwenye baraza la mawaziri ili kutoa nafasi zaidi ya uwaziri kwa ODM.

“Mabadiliko hayo yanakuja na idadi ya mawaziri kutoka Ukanda wa Mlima Kenya itapunguzwa na watasalia na wizara tatu pekee kutoka saba. Raila na Ruto wataendesha serikali kwa ushirikiano jinsi ilivyokuwa 2007,” ikaeleza duru kutoka kambi ya Raila.

Kuelezea wafuasi wake kuhusu hatua yake ya kuingia serikalini, Bw Odinga jana alikuwa Siaya na leo atakuwa Bungoma kisha Ijumaa atakuwa Busia. Katika ziara hizo, kazi kuu ni kufafanulia wafuasi wake kuwa sasa yupo serikalini hadi 2027.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*