Rais aagiza vyuo vikuu viruhusu wanafunzi wafanye mtihani – Taifa Leo


RAIS William Ruto jana alivitaka vyuo vikuu viwaruhusu wanafunzi walio na malimbikizi ya karo kufanya mitihani ya muhula huku akikiri kwamba vyuo vikuu vingi vinatatizika kifedha.

Huku akiahidi kujitolea kwa serikali kusaidia vyuo vikuu kutimiza wajibu wao wa kifedha, Rais Ruto alihusisha masaibu ya kifedha yanayovikabili vyuo vingi na kulimbikizwa kwa madeni na usumbufu uliosababishwa na mpito wa muundo mpya wa ufadhili wa elimu ya juu.

“Tunapopitia mabadiliko yaliyoletwa na muundo wa ufadhili wa elimu ya juu unaozingatia wanafunzi, nahimiza vyuo vikuu kuwa na subira na kuelewana na wanafunzi. Moyo wa kuzingatia binadamu ni muhimu hasa ikizingatiwa changamoto ya ziada inayoletwa na kesi ambayo inaweza kuvuruga utekelezaji wa muundo. Kwa hivyo, natoa wito kwa vyuo vikuu viwaruhusu wanafunzi kufanya mitihani yao ya mwisho wa muhula huku vikisubiri kurejelewa kwa malipo kamili pindi tutakapopata mwelekeo kuhusu suala hilo,” akasema akiwa Machakos mjini.

Rais Ruto alizungumza wakati alipoongoza mahafali ya Chuo Kikuu cha Scott Christian mjini Machakos. Makumi ya vijana walihitimu vyeti, stashahada na shahada baada ya kumaliza kozi za kilimo biashara, thiolojia, fiziolojia ya ushauri nasaha, usimamizi wa biashara na teknolojia ya habari na mawasiliano katika chuo hicho kinachohusishwa na AIC.

Rais Ruto alifichua kuwa baadhi ya vyuo vikuu vinakabiliwa na tishio la kufungwa kutokana na madeni makubwa. “Leo, serikali ya Kenya inadaiwa na chuo hiki zaidi ya Sh 460 milioni,” alisema.

“Najua hii imesababisha hasara kubwa kwa chuo kikuu hiki. Ndio maana nilichukua jukumu la kusuluhisha changamoto ambazo zilitatiza mfumo huo wa zamani. Mfumo wa zamani karibu ufanye vyuo vingi vifungwe. Ninafahamu kuwa chuo kikuu hiki kilifungwa kwa muda wa miezi michache. Na haikuwa sawa kwa sababu tulihusika kwa kutolipa deni kubwa la Sh 460 milioni tunalodaiwa na chuo hiki,” alisema.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*