Rais aliyebusu mchezaji wakati wa Kombe la Dunia atozwa faini ya Sh1.3milioni, akwepa jela – Taifa Leo


MADRID, UHISPANIA:

ALIYEKUWA Rais wa Shirikisho la Soka Uhispania (RFEF) Luis Rubiales amepatikana na hatia ya kudhulumu kimapenzi mchezaji wa timu ya taifa ya Uhispania, Jenni Hermoso, baada ya kumpiga busu mdomoni bila ruhusa waliposhinda Kombe la Dunia 2023.

Rubiales, 47, pia ameamrishwa na mahakama kutoenda mita 200 karibu na Hermoso, 34, wala kuwasiliana naye kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Isitoshe, Rubiales pia amepigwa faini ya Sh1,351,300 (Yuro 10,000). Aliponyoka adhabu kwa kosa jingine la madai ya kujaribu kumshinikiza Hermoso aseme kuwa alimpa ruhusa ampige busu.

Rubiales akijiandaa kumbusu mdomoni Hermoso. PICHA | MAKTABA

Viongozi wa mashtaka walitaka Rubiales afungwe jela mwaka mmoja kwa dhuluma ya kimapenzi na miezi 18 kwa madai ya kujaribu kumlazimisha Hermoso kusema busu lilikuwa la hiari. Rubiales anaruhusiwa kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

Kocha mkuu wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake ya Uhispania Jorge Vilda, mkurugenzi wa zamani wa RFEF Albert Luque na aliyekuwa afisa mkuu wa mauzo Ruben Rivera pia waliondolewa kosa la kulazimisha, baada ya kudaiwa kumwekea presha Hermoso aseme Rubiales alimbusu kwa ruhusa yake.

Hermoso alieleza mahakama juma lililopita kuwa alihisi “kutoheshimiwa” na kuwa busu hilo la lazima “lilitia doa mojawapo ya siku zake nzuri kabisa maishani.”

Presha

Uhispania ilishinda Kombe la Dunia la wanawake kwa mara ya kwanza mwaka 2023, lakini sherehe zikaharibiwa na busu hilo wakati wa kupokezwa kombe na medali.

Tabia ya Rubiales iliibua maswali kuhusu ubaguzi wa kijinsia nchini Uhispania na kufanya timu hiyo ya taifa kususia mechi za kimataifa.

Presha ilisukuma Rubiales kujiuzulu kama rais wa RFEF wiki tatu baada ya tukio hilo. Mara kadhaa alipinga madai hayo kiasi cha kudai kuwa mwathiriwa wa maonevu ya watu wanaojifanya watetezi wa haki na usawa wa wanawake.

Hermoso amesisitiza kutoka mwanzo kuwa hakumpa Rubiales ruhusa ya kumbusu, na wiki jana akasema “hangeweza kujinasua” wakati Rubiales alikuwa akimbusu.

“Sikusikia wala kuelewa chochote. Kile niliona tu ni busu limefika kwenye mdomo wangu,” alieleza korti.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Uhispania washerehekea kushinda Kombe la Dunia la Wanawake, baada ya fainali jijini Sydney, Australia, mnamo Agosti 20, 2023. PICHA | REUTERS

Hermoso alitoa ushahidi kuwa Rubiales alizungumza naye wakiwa ndani ya ndege kutoka jijini Sydney, Australia, ambako fainali ilichezewa wakirejea Uhispania.

Katika ndege hiyo, Hermoso anasema kuwa Rubiales alimuomba amsaidie kulainisha mambo kwa umma akisema watu walikuwa wakimuita “mchokozi”, lakini mchezaji huyo alikataa.

Hermoso aliongeza kusema kwamba ilikuwa muhimu kuendelea na sherehe za Kombe la Dunia na wachezaji wenzake hata baada ya tukio hilo. Lakini baada ya kurejea Uhispania maisha yake yalisimama kwa sababu ya ripoti zilizosheheni vyombo vya habari.

Mchezaji huyo anachezea klabu ya akina dada ya Tigres kwenye Ligi Kuu ya Mexico ambako anaweza kuepuka kumulikwa sana, lakini kamera hurejea kwake anaporudi jijini Madrid.

“Sijapata kuishi huru,” aliambia mahakama katika ushahidi wake.

Kabla ya adhabu ya hivi punde, Rubiales alipigwa marufuku na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kutojihusisha na soka kwa miaka mitatu. Adhabu hiyo inatarajiwa kumalizika mwaka ujao.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*