MAPEMA wiki hii, Rais William Ruto alimtembelea Rais (mstaafu) Uhuru Kenyatta katika makazi yake eneo la Ichaweri, Gatundu Kusini, Kaunti ya Kiambu.
Hatua ya Ruto kumtembelea aliyekuwa rais, haikutarajiwa kamwe na iliibua hisia mseto miongoni mwa Wakenya huku wengi wakikisia malengo ya ziara hiyo.
Kwenye taarifa ya Uhuru dakika chache tu baada ya Ruto kumtembelea, alitaja ziara ya rais kama kikao cha kawaida baina ya marais wanaohudumu na waliotangulia kwa madhumuni ya kujadili masuala muhimu ya kitaifa na ya manufaa kwa raia.
Kulingana na taarifa, Uhuru na Ruto walijadili masuala yanayohusu maslahi ya taifa pamoja, changamoto zinazokabili wananchi kama vile uhasama wa kisiasa, utozaji ushuru, ukosefu wa usalama ikiwemo mbinu bora za kusuluhisha matatizo hayo.
Suala tata kuhusu IEBC vilevile lilijitokeza ambapo Uhuru alihimiza serikali kufanya hima ili kuimarisha uadilifu wa kidemokrasia nchini.
Ziara ya Ruto imejiri wakati juhudi za baadhi ya viongozi na wanasiasa nchini za kutumia hila za kijadi za kuwagawanya Wakenya kwa misingi ya kikabila, zimeonekana kugonga mwamba.
Profesa Kithure Kindiki alipoteuliwa kuwa naibu rais baada ya Rigathi Gachagua kufurushwa afisini, hatua hiyo ilikusudiwa kugawanya Mlima Kenya mara mbili – Mashariki na Magharibi.
Juhudi hizo hazikufua dafu na badala yake, Gachagua amezidi kugeuka kipenzi cha eneo la kati ambako amekuwa akipokelewa kwa nderemo na vifijo huku mrithi wake akizidi kung’ang’ana kukumbatiwa eneo hilo na kupata umaarufu. Rais na wandani wake wamekabiliwa na wakati mgumu kuzuru Mlima Kenya hali ambayo ilichangia pakubwa ziara hiyo kwa matumani ya kutuliza hasira ya wakazi.
Haitashangaza kuona, katika siku chache zijazo, washirika wakuu wa Kenyatta wakianza kuteuliwa katika baraza jipya la mawaziri katika juhudi za kuvutia tena Mlima Kenya.
Yote haya yanajiri huku raia wakionekana kupoteza imani na viongozi hasa baada ya upinzani kusambaratishwa kupitia serikali pana iliyowezesha wandani wa Raila Odinga kupakuliwa minofu serikalini.
Hata kabla ya wananchi kupona makovu ya usaliti, mawaziri wapya kadhaa wameonekana kusahau wajibu wao na kuishia kutoa vitisho kwa raia badala ya kutilia maanani sera katika wizara zao mtawalia.
Sehemu kubwa ya Wakenya wamezinduka na hawana subira tena na sarakasi zilizopitwa na wakati ambazo zimekuwa zikitumiwa na wanasiasa kuwapumbaza raia. Ruto na viongozi kwa jumla watahitajika kujitahidi zaidi kuwashawishi Wakenya kuwa wana nia njema kwa uongozi na ustawi wa taifa.
Leave a Reply