SEOUL, KOREA KUSINI
RAIS wa Korea Kusini aliyeondolewa mamlakani Yoon Suk Yeol hatimaye Jumatano alikamatwa na kuzuiliwa huku akiendelea kuhojiwa na makachero kuhusiana na kuondoa sheria na kuwatumia wanajeshi kuwakabili waandamanaji waliokuwa wakipinga utawala wake.
Yoon ameshutumu hatua hiyo akisema alikuwa akishirikiana na vyombo vya usalama ili kuzuia ghasia. Kunyakwa kwake kumeweka historia kama rais wa kwanza wa taifa hilo kutiwa mbaroni akiwa mamlakani kisha kuhojiwa na makachero.
Korea Kusini ni kati ya nchi ambazo zinasifika kwa kuzingatia demokrasia barani Asia japo miaka ya awali imewafikisha mahakamani na kuwahukumu waliokuwa viongozi wao baada ya wao kuondoka madarakani.
Tangu wabunge wamtimue kwa makosa ya kuondoa katiba na kutumia wanajeshi kuwakabili raia mnamo Desemba 3, Yoon amekuwa akiandamwa na masaibu tele.
Amekuwa akiishi bila kutoka kwenye makazi yake ya kifahari ambayo yanalindwa na walinzi wa rais.
Mwezi uliopita walinzi hao walizuia kukamatwa kwake.
Jana, alikubali kuondoka kwenye makazi yake ili ahojiwe baada ya zaidi ya polisi 3,000 ambao walikuwa na nia ya kumkamata kutumwa makazini kwake.
“Nimekubali kuhojiwa ingawa uchunguzi wenyewe ni haramu. Nimefanya hivyo ili kuzuia umwagikaji wa damu,” Yoon akasema.
Afisa wa uchunguzi jana aliandamana na Yoon kwenye gari lake kisha wakaondoka kwenye mlango wa nyuma na kuelekea afisi za idara ya upelelezi.
Yoon alitarajiwa kuhojiwa kwa saa 48 ambapo wachunguzi wana mwanya wa kusaka hati ya kumzuilia kwa siku 20 zaidi kabla kumwaachilia.
Inadaiwa kiongozi huyo jana alikataa mahojiano yake kurekodiwa kwa kanda ya video.
Mawakili wa Yoon nao wamesema hati ya kukamatwa kwake ilitolewa na mahakama bila kufuata sheria na wachunguzi hawana mamlaka ya kumhoji.
Walinzi wa rais jana walikuwa kwenye afisi za upelelezi ambako Yoon alikuwa akichunguzwa.
Waliokuwa marais Geun-hye na bwenyenye anayemiliki Kampuni ya Elektroniki Jay Y. Lee pia waliwahi kuzuiliwa na kuhojiwa kwenye afisi hizo.
Akiwa korokoni, Yoon alitarajiwa kula chajio ambacho ni supu ya maharagwe, nyama kiasi kidogo na kabeji.
Hatua ya Yoon kuondoa katiba na kutumia wanajeshi kuliathiri uchumi wa Korea Kusini ambayo ni mshirika wa Amerika.
Wabunge walipigakura ya kumwondoa mamlakani mnamo Desemba 14.
Kando na uchunguzi wa idara ya upelelezi, Mahakama ya Kikatiba inashughulikia kesi ambayo itahalalisha au kuharamisha kutimuliwa kwake afisini.
Afisi ya Msemaji wa Baraza la Kitaifa la Usalama kwenye Ikulu ya White House kupitia taarifa ilisema walikuwa wakifuatilia yanayoendelea Korea Kusini kwa jicho la ndani.
Taarifa hiyo ilisema Amerika inatambua na kuwaheshimu juhudi za raia na vyombo husika katika kufuata sheria kushughulikia utata huo wa kisiasa.
Msemaji wa serikali katika taifa jirani la Japan Yoshimasa Hayashi pia alisema wanafuatilia kwa jicho la ndani mkwamuo huo wa kisiasa huku wakiwa na matumaini sheria itafuatwa.
Leave a Reply