KIFO cha wakili Mkuu wa haki na masuala ya familia Judy Thongori ni pigo kubwa kwa nchi ya Kenya na taaluma ya uanasheria, viongozi na mawakili wenzake wamesema.
Rais William Ruto alimteua katika jopokazi la kukagua sekta ya kidini mnamo 2023.
Jopokazi lililoongozwa na Mutava Musyimi lilikuwa miongoni mwa mengine, liandae mapendekezo kuhusu elimu ya uraia na nyongeza katika mitaala ya elimu ambayo itawahamasisha Wakenya kutambua, kuepuka au kuacha madhehebu na mashirika yenye itikadi kali za kidini.
Bw Musyimi, aliyeongoza jopokazi hilo alisema kuaga dunia kwa Bi Thongori ni hasara kubwa kwa nchi.
Alisema Bi Thongori alikuwa muhimu katika timu hiyo ilipozunguka nchi nzima kukusanya maoni kutoka kwa Wakenya.
“Alikuwa msikilizaji makini na mwenye shauku kuhusu jukumu lake. Alikuwa mchapakazi, mvumilivu na alisaidia jopo kazi katika masuala ya kisheria,” alisema.
Wakili Dorcas Mwae alisema Bi Thongori alionyesha heshima kwa wote, bila kujali umri au cheo.
“Alionyesha heshima mahakamani na nje ya chumba cha mahakama. Alikuwa na heshima alipofika mbele ya hakimu mkazi hadi katika Mahakama ya Juu,” Bi Mwae alisema.
Wakili huyo alifichua kwamba alijifunza kutoka kwa Bi Thongori jinsi ya kuandaa Wosia wakati wa mafunzo ya kukuza taaluma ya uwakili yanayoendeshwa na Chama cha Wanasheria ili kukuza ujuzi wao na maarifa ya sheria.
Bi Mwae alisema Bi Thongori alishughulikia mada zake kuhusu sheria ya familia kwa njia rahisi.
Bi Thongori alifariki alipokuwa akipokea matibabu nchini India, kulingana na taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa Wakili Mkuu (SCB) Fred Ojiambo.
Taarifa hiyo ilisema Bi Thongori aliugua hivi majuzi, na alisafirishwa hadi India kwa matibabu ya dharura.
“Cha kusikitisha ni kwamba alifariki Jumanne jioni kutokana na matatizo ya kiafya,” Dkt Ojiambo alisema.
Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula alimtaja Bi Thongori kama mfuasi wa sheria za familia, na kwamba alijitolea sio tu kuendeleza sheria katika nyanja hiyo, bali pia kulea kizazi kijacho cha wanasheria.
“Ushauri wake kwa mawakili wachanga, haswa kushughulikia utata wa sheria za familia, ni urithi ambao utadumu kwa miaka ijayo,” alisema.
Jaji Mkuu Martha Koome alimsifu Bi Thongori kama mtetezi wa haki, hasa katika masuala yanayohusu familia, wanawake na watoto.
“Tulifanya kazi kwa karibu wakati wetu katika Fida-Kenya, ambapo nilihudumu kama Mwenyekiti, na aliongoza Idara ya Sheria kwa ari na ustadi usio na kifani mwishoni mwa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000,” Jaji Koome alisema.
Jaji Koome aliongeza kuwa uongozi wa Bi Thongori ulichangia pakubwa katika kuiweka Fida-Kenya nguvu katika kutumia sheria kulinda haki, maslahi, na utu wa wanawake, watoto na ustawi wa familia zilizo katika mazingira magumu.
CJ Koome aliongeza kuwa baada ya muda wake katika FIDA-Kenya, Bi Thongori alianza kazi ya kibinafsi ya uwakili, ambapo alipata umaarufu kama mmoja wa wataalamu wa sheria za familia nchini.
Leave a Reply