MIAMBA wa Uhispania, Real Madrid wamekuwa klabu ya kwanza kabisa ya soka kuwa na mapato ya zaidi ya Sh134.7 bilioni (Yuro 1bilioni) kwa mwaka, tathmini ya kampuni ya Deloitte inasema.
Real wamesalia kileleni mwa ligi hiyo kifedha ya Deloitte wakiwa na mapato ya Sh141.4 bilioni (Yuro 1.05 bilioni) kutoka msimu wa 2023-2024 ambapo walitawala Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).
Manchester City pia wamekwamilia nafasi ya pili wakiwa na mapato ya Sh112.9 bilioni (Yuro 838 milioni). City walinyakua taji la nne mfululizo la Ligi Kuu ya Uingereza, Klabu Bingwa Duniani, na Uefa Super Cup msimu jana.
Paris Saint-Germain (Sh108.5 bilioni), Manchester United (Sh103.8 bilioni) na Bayern Munich (Sh103.0 bilioni) wanafunga nafasi tano za kwanza kwenye ligi hiyo. Aston Villa wako ndani ya 20-bora baada ya kushiriki mashindano ya Ulaya kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2011.
Klabu tisa kutoka Ligi Kuu ya Uingereza zinasalia ndani ya 20-bora. Arsenal wamepaa kutoka nafasi ya 10 hadi saba wakiwa na mapato ya Sh96.6 bilioni, nao Liverpool, Tottenham Hotspur na Chelsea wako chini nafasi moja hadi nambari nane, tisa na 10 wakiwa na mapato ya Sh96.3 bilioni, Sh82.8 bilioni na Sh73.5 bilioni, mtawalia.
Newcastle wameruka juu nafasi mbili na kutulia katika nafasi ya 15 kwa Sh50.1 bilioni nao West Ham wamepaa nafasi moja hadi nambari 17 wakiwa na mapato ya Sh43.3 bilioni. Villa ni nambari 18 kwa mapato ya Sh41.7 bilioni.
Lyon ni timu nyingine pekee mpya ndani ya 20-bora ikiwa na Sh35.5 bilioni. Kuingia kwa Villa na Lyon katika mduara wa 20-bora kumesukuma nje Napoli na Eintracht Frankfurt.
Brighton, Crystal Palace, Everton, Fulham na Wolves wanapatikana katika nafasi ya 21, 26, 27, 28 na 29, mtawalia.
Mapato ya 20-bora yaliongezeka kwa asilimia sita na kufikia Sh1.55 trilioni. Mapato ya siku ya mechi yalionyesha ukuaji wa haraka baada ya kuongezeka kwa asilimia 11 na kufika Sh282.2 bilioni.
Yalichangiwa pakubwa na ongezeko na idadi ya viti katika uwanja, bei ya tiketi na huduma za kipekee kwa mashabiki wanaonunua tiketi zisizo za mashabiki wa kawaida.
Real wamenufaika pakubwa na ongezeko la mapato ya siku ya mechi, wakipata Sh33.4 bilioni – maradufu ya mwaka uliotangulia – baada ya kukarabati uwanja wa Santiago Bernabeu.
Barcelona wako chini nafasi mbili hadi nambari sita baada ya kupoteza mapato ya siku ya mechi kwa Sh8.4 bilioni kwa sababu ya kuhamishia mechi zao katika uwanja mdogo wakati Camp Nou inarekebishwa.
Mapato kutokana na biashara yalisalia kuwa njia kuu kwenye ligi hiyo ya kifedha, yakiimarika kwa asilimia 10 hadi Sh703.1 bilioni na kuchangia asilimia 44 ya mapato yote, yakisaidiwa pakubwa kwa kuandaa hafla moja kwa moja zisizo za kimichezo zikiwemo tamasha.
Mapato yanayotokana na kupeperushwa kwa mechi yalisalia Sh580.3 bilioni katika ligi tano kubwa – Uingereza, Uhispania, Ujerumani, Ufaransa na Italia.
Tathmini ya Deloitte kuhusu klabu 15 za wanawake zinazoongoza katika mapato ulionyesha jumla ya mapato zaidi ya Sh15.9 bilioni ambayo ni ongezeko la asilimia 35 hadi Sh15.6 bilioni.
Barcelona wanaongoza kwa mwaka wa tatu mfululizo wakiwa na mapato yaliyoongezeka kwa asilimia 26 hadi Sh2.4 bilioni.
Arsenal wamerukia nafasi ya pili kutoka nambari tano wakiwa pia na Sh2.4 bilioni baada ya ongezeko la asilimia 64 ya siku ya mapato hadi Sh685.6 milioni.
Kuandaliwa kwa mashindano ya Supa Ligi ya Wanawake ya klabu six-bora (WSL) ugani Emirates kulichangia katika kuongezeka kwa mapato ya kinadada wa Arsenal.
Chelsea wanakamata nafasi ya tatu (1.8 bilioni) na kufuatiwa na Manchester United (Sh1.43m) na Real Madrid (Sh1.41 bilioni).
Leave a Reply