Riggy G ni mtu wangu, tungali marafiki, asema Kindiki – Taifa Leo


KWA mara ya kwanza Naibu Rais Kithure Kindiki amefunguka kuhusu uhusiano wake na mtangulizi wake Rigathi Gachagua akisema wanasalia kuwa marafiki wa dhati.

Kindiki ambaye alizungumza katika kikao cha wanahabari siku ya Alhamisi alisema uhusiano wao haujabadilika hata kidogo.

“Uhusiano wetu ni sawa na ulivyokuwa. Sisi ni marafiki wazuri, “alisema.

Alipoulizwa kuhusu alilojifunza kutokana na muhula wa Gachagua, Kindiki alisema hataki kumjadili Naibu Rais huyo wa zamani.

Alisisitiza kuwa itakuwa vibaya kwake kuanza kujilinganisha na Gachagua.

“Niruhusu nisimjadili kaka yangu Rigathi Gachagua. Ni makosa kuanza kujilinganisha na mtu aliyekuwa akishikilia ofisi hii,” alisema.

Kuhusu iwapo mchakato wa kumtimua Gachagua ulikuwa na dosari, Kindiki alisema kuwa mchakato huo ulihusisha mihimili yote ya serikali na haoni tatizo nalo.

“Mchakato huo ulihusisha mihimili mitatu ya serikali, Serikali Kuu,Bunge na Mahakama. Sioni tatizo na mchakato huo,” Profesa Kindiki alisema. Kuhusu iwapo anajuta kuchukua kazi hiyo, Kindiki alisema kuwa hana majuto hata kidogo. “Sijutii kuchukua nafasi hii (kuwa Naibu Rais).”

Rais William Ruto alimteua Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais kufuatia kuondolewa kwa Rigathi Gachagua.

Alimtaja Naibu Rais mpya kuwa mtumishi wa umma asiyechoka katika uongozi wa kitaifa.

Ruto alisema Kindiki ni mzalendo ambaye kujitolea kwake kwa uwiano, umoja wa kitaifa na ushirikishaji hauna doa.

 

 

 

 

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*