WENGI wa wakazi wa Kisumu wameeleza imani yao kuwa Kinara wa Upinzani Raila Odinga atatamba kwenye uchaguzi wa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) wikendi, baadhi wakisema wadhifa huo ni mkubwa hata kuliko urais.
Bw Odinga aliwania urais 1997, 2007, 2013, 2017 na 2022 lakini hajawahi kufanikiwa, wengi wa wafuasi wake wakiamini amekuwa akichezewa shere katika kura nne zilizopita.
Kisumu na ngome za Bw Odinga za Nyanza, Magharibi na Pwani, zimekuwa zikimwombea dua waziri huyo mkuu wa zamani huku baadhi ya wakazi wakisema wadhifa huo wa AUC ni mkubwa hata kushinda Urais ambao Raila ameusaka bila mafanikio miaka mingi.
Mji huo wenye shughuli nyingi umeonekana kutekwa na siasa za AUC wakazi wakinongónezana iwapo kutakuwa na mlipuko wa furaha Jumamosi au wimbi la simanzi litawanyanyasa moyoni jinsi ambavyo imekuwa kila matokeo ya urais yanapotangazwa.
“Raila Odinga amezuru mataifa ya Afrika akifanya kampeni na tuna imani atashinda wadhifa huo,” akasema John Otieno, mkazi wa Kisumu.
Kauli yake iliungwa mkono na Evance Otieno ambaye pia anaamini Raila anatosha kwa kazi hiyo.
“Kutokana na uzoefu wake wa miaka mingi, Raila ameonyesha kuwa ni kiongozi bora na anatoshea wadhifa huu ambao ni zaidi ya urais. Nina hakika atatamba Jumamosi,” akasema Bw Otieno.
Ingawa hivyo, baadhi ya wakazi bado wana hatihati na ushindi wa Raila hasa baada ya matumaini yao kuwa angeshinda urais chaguzi zilizopita na akaishia kubwagwa.
“Tunaombea ushindi wa Raila ila pia tunatambua kuwa katika uchaguzi wowote kuna kushinda na kushindwa. Hata Raila mwenyewe ametuhakikishia kuwa atakubali matokeo,” akasema Bw Onyango.
Bw Odinga atapambana na Waziri wa Masuala ya Nje wa Djibouti Mahmoud Ali Youssouf pamoja na aliyekuwa Waziri wa Kigeni wa Kisiwa cha Madagascar Richard James Randriamandrato.
Ngome za Bw Odinga zimekuwa zikifanya maombi, baadhi ya wafuasi wake wakifunga ili mara hii afanikiwe ikizingatiwa sasa amekweza ngazi na kujiunga na siasa za Afrika.
Rais William Ruto ambaye amekuwa mstari wa mbele kurindima ngoma ya ‘Baba’ anatarajiwa kuondoka nchini Jumatano jioni kuelekea Addis Ababa ambako kura hiyo itaandaliwa mnamo Jumamosi.
Leave a Reply