Ruto ahofia Kenya itapoteza maadili yake kufuatia matumizi mabaya ya mitandao – Taifa Leo


RAIS William Ruto ameelezea wasiwasi kuwa taifa la Kenya liko kwenye hatari ya kupoteza maadili yake iwapo Wakenya wataendelea kutumia vibaya mitandao ya kijamii.

Kiongozi huyo wa taifa ameelezea kusikitishwa kwake na baadhi ya Wakenya, aliosema wanatumia mitandao ya kijamii vibaya ili kukuza tabia zinazokinzana na jamii ambazo zinamomonyoa maadili.

Kwenye hotuba aliyoitoa Mkesha wa Mwaka Mpya katika Ikulu Ndogo ya Kisii, Rais Ruto alisema udumishaji wa maadili katika jamii ni suala linalohitaji juhudi za washikadau wote.

Kauli ya Dkt Ruto inajiri wakati visa vya utekaji nyara vinazidi kuongezeka nchini, ambapo vijana wanaoonekana kuukosoa utawala wake wanakamatwa na kulazimishwa ndani ya magari kutokomezwa kusikojulikana na watu wanaoaminika kuwa maafisa wa polisi.

Wengi wa vijana hao wametoweka kwa siku kadhaa sasa na inasemekana watekaji hao wanatumia mbinu hiyo ili kuwanyamazisha wasiendelee na mazoea yao ya kumkosoa Rais.

Hali hiyo imewaacha ndugu, jamaa na marafiki wa vijana hao na simanzi chungu nzima wakihofia uhai wao.

Hali hiyo imesababisha ghadhabu ya umma na miito ya kutaka vijana hao wapewe uhuru wao ikitolewa kutoka kila pembe ya nchi.

Polisi hata hivyo, kupitia Inspekta Jenerali Douglas Kanja wamekana kuhusika na utekaji nyara huo.

Ili kukomesha tabia hiyo isiyofaa, Rais Ruto aliomba mashirika ya kidini, sekta ya elimu, na taasisi za sheria na utaratibu kuunga mkono na kukamilisha jukumu la kimsingi la familia katika kulea raia wenye huruma, wanaowajibika na waliopewa mamlaka ya kuendeleza nchi mbele.

“Kama jamii, tuna matarajio halali kwamba vizazi vijavyo, vikinufaika na mkusanyiko wa maendeleo ya kijamii, kiuchumi, kisayansi na kiteknolojia, vitaleta nishati kubwa, mawazo bora, maono yaliyo wazi zaidi, na kujitolea kwa nguvu kwa maadili yetu ya pamoja. Tunapaswa kuwa raia wenye utu, uwajibikaji, na wenye misingi mizuri ambao matendo yao yanakuza umoja, uzalendo, demokrasia, utawala wa sheria, na haki na uhuru wetu, badala ya kuzihujumu,” rais Ruto alisema.

Aliwaomba wazazi wasiliasi jukumu lao la kuwalea wana wao kwa njia sahihi.

“Hili ni muhimu, kwani mabadiliko yote tunayofanya leo hayatakuwa na maana yoyote ikiwa vijana wetu wataachwa bila mwongozo mzuri, ushauri wa maadili na usaidizi wa kimaadili,” Rais Ruto aliongeza.

Dkt Ruto aliongeza kuwa ataendelea kutoa mwaliko kwa washikadau wote katika kujiunga kwenye mazungumzo ya kitaifa, ya kutafuta njia bora za kutekeleza mkakati wa jamii yote na mbinu ya kukabiliana na upotovu wa maadili na kuweka upya dira ya maadili nchini.

Alipigia debe serikali yake pana, na kusema ataendelea kufanya mazungumzo ya kitaifa na viongozi kutoka makundi mbalimbali ya kisiasa ili kupanua kanuni ya ushirikishwaji bila kuathiri maadili ya msingi ya demokrasia ya ushindani na mitazamo tofauti.

“Lengo letu ni kukuza, na sio kupunguza, utambulisho wetu kama jamii huru, wazi na ya kidemokrasia iliyojengwa kwa misingi ya katiba na sheria. Tunafanya maendeleo ya maana, ambayo yakidumishwa, yatatuweka kama demokrasia iliyokomaa iliyo na msingi thabiti. katika utamaduni endelevu wa kisiasa” Dkt Ruto alisema.

Aliwasifu Wakenya kwa kusimama kidete mwaka wa 2024 na kuwataka waendelee kuwa wastahimilivu zaidi katika mwaka mpya wa 2025.

“Taifa letu lilikabiliwa na changamoto kubwa na matatizo makubwa. Hata hivyo, tulifanya zaidi ya kuvumilia; tulisimama pamoja kwa umoja, tulifanya kazi kwa dhamira, na kushinda vizuizi hivi. Kwa sababu sisi ni Wakenya, watu wasiokata tamaa, jasiri na wasioogopa kufanya kazi kwa bidii , kwa sababu sisi ni mabingwa hodari ambao tunajitahidi kushinda na kukabiliana na kila changamoto kwa kujitolea, tulipata maendeleo licha ya matatizo makubwa,” Rais alisema.

Dkt Ruto aliwataka Wakenya kuangazia mwaka mpya kwa matumaini na kujitolea upya, sio tu kufanya kazi kwa bidii na kupata maendeleo makubwa zaidi bali pia kujibadilisha na kubadilisha kila changamoto kuwa fursa.

“Ifikapo mwaka 2025, mbegu tulizozipanda kwa subira na umakini zitaendelea kuota na kukua. Hatua tuliyofikia imetuweka kwenye njia ya ukuaji wa haraka na endelevu. Kutokana na hali hiyo, tunaweza kutarajia ufanisi mkubwa wa kiuchumi, ajira zaidi. kwa vijana wetu, na mapato ya juu kwa wakulima na wajasiriamali,” Rais alisema.

Rais alikiri visa vya mauaji ya kiholela yanayofanywa na maafisa wa usalama.

Alisema taratibu zinaendelea katika taasisi zinazostahili ili kuhakikisha uwajibikaji.

Hata hivyo alitahadharisha Wakenya kwamba uhuru wao una mipaka na kwamba usalama na utulivu wa umma lazima kila wakati uondoe tamaa ya uhuru usiodhibitiwa.

“Lazima tuhakikishe kwamba kufuata kwetu haki na uhuru hakuathiri usalama wetu wa pamoja au wa mtu binafsi. Tusiwaruhusu wahalifu kutumia haki za kikatiba kuwadhuru na kuwaangamiza wengine,” Dkt Ruto alibainisha.

Mke wa Rais Rachel Ruto, viongozi wakuu wa serikali, viongozi wa eneo la Gusii na wageni wengine waalikwa waliungana na rais katika kukaribisha mwaka mpya katika ikulu hiyo ndogo.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Rais aliye madarakani wa Kenya kuhutubia taifa katika mkesha wa mwaka mpya nje ya miji mikuu.

Gavana wa Kisii Simba Arati na Seneta Richard Onyonka hawakuhudhuria hafla hiyo. Seneta Onyonka alikataa mwaliko wa kupamba sherehe hizo, akitaja kuwa utawala wa Kenya Kwanza umeshindwa kukomesha ongezeko la visa vya utekaji nyara miongoni mwa sababu nyinginezo.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*