RAIS William Ruto amewashutumu magavana kwa kudai walitia saini zabuni ya ukodishaji wa vifaa vya kimatibabu kwa kulazimishwa na bila kuifahamu.
Haya yanajiri siku moja baada ya Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Mutahi Kahiga kuiambia Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu (CPAC) kwamba magavana waliwekwa gizani kuhusiana na zabuni hizo za kuwasilishwa kwa vifaa hivyo katika hospitali za kaunti chini ya Mpango wa Kitaifa wa Utoaji wa Vifaa vya Kimatibabu (NESP).
Bw Kahiga pia aliiambia kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang, kwamba serikali za kaunti hazikuhusishwa katika usakaji wa kampuni za kuwasilisha vifaa hivyo.
Hata hivyo, akiongea kaitka kaunti ya Kilifi jana, Rais Ruto aliwashambulia magavana hao akisema kila kitu kilichohitajika kwa vifaa hivyo kilikadiriwa bei na wataalamu na serikali ya kitaifa na zile za kaunti ziliwakilishwa.
“Serikali za kaunti na Wizara ya Afya ziliwakilishwa katika mchakato wa utoaji zabuni. Hamna serikali yoyote ya kaunti ilipaswa kupata vifaa vyovyote moja kwa moja kutoka kwa kampuni yoyote,” Dkt Ruto akasema, akionekana kuanzissha mvutano kati ya serikali kuu na magavana.
Akaendelea kusema: “Mtu yeyote anayedai kuwa walilazimishwa na serikali ya kifaifa kutia saini kandarasi yoyote ni wao na matapeli. Ikiwa utalazimishwa kutia saini chochote na ukafanya hivyo basi wewe ni mjinga.”
Rais Ruto alisema kuwa serikali za kaunti zilikuwa na uhuru wa kuchagua vifaa ambavyo walihitaji.
Kiongozi wa taifa alikuwa akiongea alipoongoza ufunguzi rasmi wa Kongamano la Kimataifa ya Uwekezaji la Kaunti ya Kwale lililoanza Alhamisi.
Alihakikishia umma kwamba ufisadi na ulaghai hautaruhusiwa chini ya utawala wake haswa katika sekta ya afya.
Kulingana na Dkt Ruto serikali ya kitaifa imejitolea kuhakikisha kuwa Wakenya wanafaidi kutoka na pesa wanazochanga katika Bima ya Afya ya Kijamii (SHIF) bila kutokea kwa sakata zozote kama zile zilizoshuhudiwa chini ya Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) ilifutiliwa mbali.
“Nitawaangalia Wakenya machoni na kuwaambia kwamba ufisadi hautaruhusiwa kutokea katika sekta ya afya wakati huu ambapo mimi ni Rais. Sharti tumalize ulaghai na kuwahakikishia Wakenya kuwa pesa zote wanazolipa zinawafaidi wala sio watu fulani wafisadi,” akaeleza.
Kamati ya CPAC kwenye kikao chake cha Jumanne wiki kilionya kuwa huenda mpango wa NESP ukaishia kuzongwa na ufisadi sawa na mpango wa Medical Equipment Services (MES) iliyogharimu Sh63 bilioni.
Lakini japo, serikali za kaunti zililipia vifaa vya kisasa chini ya mpango wa MES, baadhi ya vifaa hivyo havikuweza kutumika kwa sababu hakukuwa na wataalamu wa kuvitumia.
Matokeo yake ni kwamba serikali za kaunti ziliendelea kulipia vifaa na mitambo hiyo kwa kima cha Sh200 milioni kwa mwezi ilhali hazikufaidi raia.
Leave a Reply