Ruto aleta watetezi wapya wa serikali yake kwa kuteua washirika wa Uhuru – Taifa Leo


WASHIRIKA wa karibu wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, Mutahi Kagwe na Lee Kinyanjui na aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo wameteuliwa mawaziri katika mabadiliko ambayo Rais William Ruto alifanya Alhamisi.

Bw Kagwe, ambaye alihudumu kama waziri wa afya katika serikali ya Uhuru Kenyatta, ameteuliwa waziri wa Kilimo na Ustawi wa Mifugo huku Bw Kinyanjui ambaye alikuwa gavana wa Nakuru kati ya 2017 na 2022 akiteuliwa waziri wa Biashara na Uwekezaji na Viwanda.

“Kwa mujibu wa Kifungu cha 152 (2) cha katiba Mheshimiwa Rais amewateua watu wafuatao kuteuliwa kuwa Mawaziri: Mutahi Kagwe na William Kabogo,” taarifa kutoka Ikulu ilisema.

Bw Salim Mvurya ambaye alikuwa waziri wa Biashara, Uwekezaji na Viwanda amehamishiwa wizara ya Michezo na Vijana huku Dkt Andrew Karanja ambaye alikuwa waziri wa Kilimo akiteuliwa balozi wa Kenya nchini Brazil.

Bw Kabogo ambaye chama chake cha Tujibebe Wakenya ni sehemu ya muungano tawala wa Kenya Kwanza, aliteuliwa waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi Dijitali kuchukua nafasi ya Dkt Margaret Nyambura Ndung’u ambaye ameteuliwa balozi wa Kenya nchini Ghana.

Mshirika mwingine wa karibu wa Bw Kenyatta, Ndiritu Muriithi ambaye alikuwa gavana wa Laikipia na ambaye alitarajiwa kukabidhiwa uwaziri, aliteuliwa mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA) kuchukua nafasi ya Antony Mwaura ambaye amehamimishiwa bodi ya Mamlaka ya Barabara za Mashambani.

Aliyekuwa seneta wa Murang’a Bw Kembi Getura aliteuliwa mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Rais Ruto alisema kwamba, mabadiliko hayo ambayo yalijiri wiki moja baada ya handisheki yake na Bw Kenyatta alipomtembelea nyumbani kwake Ichaweri yananuiwa kuimarisha utoaji wa huduma.

Kulingana na Rais, hatua ya kufanya mabadiliko hayo inalenga kurekebisha Wizara ili kuboresha utendakazi na kuimarisha utoaji wa huduma kama ilivyoainishwa katika mpango wa Utawala wa Kenya Kwanza chini ya Ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi ya kuanzia mashinani.

Katika mabadiliko hayo, Rais Ruto alimhamisha mwandani wake Onesmus Kipchumba Murkomen kutoka wizara ya Michezo na Vijana kusimamia wizara yenye nguvu ya Usalama wa Ndani iliyoachwa wazi Profesa Kithure Kindiki alipoteuliwa naibu rais.

Wizara hiyo imekuwa ikishikiliwa na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi tangu Profesa Kindiki alipoteuliwa naibu rais kuchukua nafasi ya Gachagua.

Aliyekuwa waziri wa Michezo na Masuala ya vijana katika baraza la kwanza la mawaziri la Rai Ruto, Ababu Terah Namwamba aliteuliwa balozi wa Kenya katika Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (UNEP) lenye makao makuu Nairobi.

Kwa kuteua washirika wa Bw Kenyatta katika Serikali yake, Rais Ruto anaonekana kulenga kukomboa ushawishi wake katika eneo la Mlima Kenya ulioyeyuka baada ya kutimuliwa kwa Rigathi Gachagua aliyekuwa naibu rais.

Hata hivyo,Bw Gachagua amesema ukuruba wa Dkt Ruto na Kenyatta hautaathiri kwa vyovyote mwelekeo wa kisiasa anaolenga kutoa Januari kwa wakazi wa Mlima Kenya.

Mbunge huyo wa zamani wa Mathira, ambaye aliondolewa afisini Oktoba, ameahidi wafuasi wake kuwa atatoa tangazo kuu la kisiasa mapema mwakani.

“Hatuwezi kuwazuia watu kukutana. Hatuwezi kuamua nani anakutana na yupi nyakati hizi. Hatuna mamlaka kama hayo. Ama kwa hakika tunahimiza watu wengi waje pamoja na wazungumze kwa manufaa yao. Sisi pia tunaongea lakini kuna masuala tunayozungumzia ambayo tumeamua yawe siri,” Bw Gachagua akasema kwenye mahojiano na Taifa Leo wiki jana

Baada ya mkutano wa Uhuru na Ruto, ilisemekana mabadiliko yalitarajiwa serikalini kujumuisha washirika wa rais huyo wa nne wa Kenya ambayo majina ya Kagwe, Ndiritu na Kinyanjui yalitajwa.

“Hivi karibuni utawaona wandani wa Bw Kenyatta wakitunukiwa vyeo serikalini Rais Ruto akijaribu kurejesha ushawishi wake kisiasa Mlima Kenya.” Mchanganuzi wa siasa Profesa Peter Kagwanja alisema wiki jana.

“Rais Ruto alipozomewa mwezi jana katika kaunti ya Embu, aligundua kuwa Bw Gachagua na Bw Kenyatta walishangiliwa. Kwa sababu hawezi kupatana na Bw Gachagua sasa, rais ameona ni hatua ya busara kuzungumza na Bw Kenyatta,” Profesa Kagwanja alieleza.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*