
HADHI ya Kinara wa Upinzani Raila Odinga katika siasa za Kenya zilidhihirika jana, wakati ambapo Rais William Ruto na Naibu wake Profesa Kithure Kindiki walipompaka mafuta kwa kumrejelea kama ‘waziri mkuu’ katika hotuba zao.
Bw Odinga jana alirejea nchini na kufululiza hadi Pwani ya nchi ambapo alikaribishwa na Rais Ruto na Profesa Kindiki katika ikulu ya Mombasa.
Raila alirejea nchini wiki mbili baada ya kulemewa kwenye kura za AUC na Waziri wa Masuala ya Nje wa Djibouti Mahmoud Youssef licha ya kuendesha kampeni kali na kuzunguka kote Afrika.
Rais William Ruto alimrejelea Raila kama ‘waziri mkuu’ kwenye hotuba yake yote huku Profesa Kindiki pia akimrejelea kwa jina hilo hilo katika mazungumzo yake.
Raila alikuwa katika ikulu ili kumshukuru Rais Ruto na utawala wake kwa kuunga mkono azma yake na kugharimia kampeni zake kote Afrika alipokuwa akisaka kiti cha AUC.
Kwa kawaida, wakati ambapo huwa kuna cheche kali za kisiasa nchini, wawili hao wamekuwa wakimrejelea Raila kama ‘aliyekuwa waziri mkuu’ lakini jana mambo yakawa tofauti.
“Tunashukuru Mungu hata baada ya AUC, Rais na Raila wameendelea kushirikiana. Nachukua fursa hii kukushukuru Rais na Waziri Mkuu Raila Odinga hata kama hatukushinda AUC. Bado mnaendelea kushirikiana na viongozi wengine. Karibu mheshimiwa waziri mkuu Raila Odinga uhutubu kisha ualike Rais,” akasema Profesa Kindiki.
Mara nyingi katika hafla za umma, huwa Profesa Kindiki ndiye humwalika Rais kuhutubu lakini jana alimwaachia Raila jukumu hilo, ishara kuwa ushirikiano kati ya Raila na Ruto umenoga.
Aliposimama kuhutubu, Rais Ruto alimrejelea Raila kama waziri mkuu kwenye hotuba yake yote ambapo alimsifu kwa kupambana kishujaa licha ya kushindwa.
“Nataka nisisitize maneno ambayo yamesemwa na Naibu Rais na waziri mkuu Raila Odinga kuwa tulikuwa na mwaniaji bora AUC,” akasema Rais Ruto.
“Waziri Mkuu Raila Odinga alipotangaza kuwa anataka kuwania cheo hicho, tuliwasilisha uwanizi wake kupitia baraza la mawaziri ambalo liliamua kuwa serikali ingedhamini shughuli zote,” akasema Rais.
Mjadala kuwa Raila anapangiwa wadhifa wa waziri mkuu au cheo cha hadhi, umekuwa ukiendelea nchini huku baadhi ya wandani wa Raila na Rais Ruto wakisema hawezi kuachwa ‘akae’ bure baada ya kushindwa Afrika.
Mbunge wa Belgut Nelson Koech alinukuliwa akisema utawala wa Kenya Kwanza hauna shida iwapo Bw Odinga atutuzwa nafasi ya kutumikia serikali baada ya kuanguka AUC.
“Tunaweza kufanya vyema zaidi iwapo tutakuwa na afisi ya waziri mkuu itakayoongozwa na Raila Odinga,” akasema Koech.
Jana, duru ziliarifu kuwa Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka huenda akakutana na Raila pia hii leo.
ODM inatarajiwa kuandaa mkutano hapo kesho ambapo duru zinaarifu suala la Raila kufanya kazi na Rais Ruto litaidhinishwa kwa mara nyingine, hoja kuu ikiwa ni nafasi ambayo kiongozi huyo wa upinzani atachukua serikalini.
Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati, suala kuu kwa mrengo wa Kenya Kwanza ni jinsi ambavyo Raila ataingizwa serikalini bila kumkwaza Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi.
“Wengi katika ODM wanataka Raila atafutiwe cheo lakini sasa hilo linamweka Musalia wapi? Kumbuka kuwa kubuni nafasi ya waziri mkuu kupo kwenye ripoti ya NADCO lakini pia nayo lazima ipitishwe kwenye kura ya maamuzi,” akasema Bw Andati.
Leave a Reply