Ruto apenya katika‘Bedroom’ ya Raila – Taifa Leo


ZIARA za hivi majuzi za Rais William Ruto katika ngome za chama cha Orange Democratic Movement (ODM) cha Raila Odinga zimeibua uvumi kuhusu juhudi zake za kuimarisha ukuruba wao mpya wa kisiasa kabla ya uchaguzi wa mwaka wa 2027.

Haya yanajiri Dkt Ruto akionekana kutochangamkiwa na baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya, baada ya kutimuliwa kwa aliyekuwa naibu wake Rigathi Gachagua.Maeneo ya Pwani, Nyanza na Magharibi yamekuwa ngome kuu za upinzani kwani ODM imekuwa ikijizolea kura nyingi katika uchaguzi mkuu ukiwemo wa 2022.

Wiki hii pekee, Rais alizuru kaunti tatu za Pwani na ingawa ziara hizo zilikuwa rasmi, hazikukosa ‘ladha’ ya kisiasa. Alhamisi, Rais alikuwa Kilifi kufungua rasmi Kongamano la Kimataifa la Uwekezaji la Kilifi lililofanyika Vipingo.

Ziara hiyo ilijiri siku mbili tu baada ya ziara yake ya siku mbili katika Kaunti ya Taita Taveta, ambapo alizindua miradi kadhaa ya maendeleo na kuongoza hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha kuchakata chuma cha Sh11 bilioni Manga, Voi.

Dkt Ruto pia anatarajiwa kufungua rasmi Michezo ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Kaunti ya Mombasa kuanzia jana Ijumaa hadi Desemba 18.

Mapokezi mazuri

Ziara hizi katika eneo la Pwani zilijiri wiki moja tu baada ya kukaribishwa kwa kishindo katika Kaunti ya Kisumu, ambayo ni ngome kuu ya kisiasa ya Bw Odinga.Pia, alikuwa amefanya mkutano na viongozi wa kisiasa wa Pwani katika Ikulu mapema Novemba 25.

Kulingana na wachanganuzi wa masuala ya kisiasa, ziara hizi, ingawa zimepangwa kama ziara rasmi, zimethibitisha waziwazi kuwa ni mkakati wa kisiasa kutokana na hotuba za viongozi kadhaa.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa waliozungumza na Taifa Leo walisema Rais anaweza kupata uungwaji kutoka maeneo haya kwa matumaini ya kuunda muungano na chama cha ODM katika siku zijazo.

Katika mkakati huo, Rais Ruto anaonekana kulenga kuvutia wakazi katika ngome za waziri mkuu huyo wa zamani baada ya kumvuta Bw Odinga upande wake, na kuchangamkiwa na viongozi wengine wa ODM.

Hii, kwa wadadisi wa kisiasa, ni hatua ya kimkakati hasa baada ya kutimuliwa kwa Bw Gachagua, jambo ambalo limewasumbua baadhi ya wafuasi wa Dkt Ruto ambao walichangia pakubwa katika kuchaguliwa kwake katika Mlima Kenya.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Sammy Ruwa alisema kujitosa kwa Rais Ruto Pwani na Kisumu ni sehemu ya mikakati yake ya kupata ufuasi kutoka kwa maeneo mbalimbali kwa kuwa anaonekana kupoteza Mlima Kenya.

“Rais karibu amepoteza eneo muhimu ambalo ni Mlima Kenya na anahitaji kutafuta njia ya kupata msaada kutoka maeneo ambayo hayakumuunga mkono na pwani ni moja. Bila shaka anapenya Pwani na Nyanza kuona ikiwa anaweza kuziba pengo ambalo liliachwa na Naibu Rais aliyetimuliwa,” akasema Bw Ruwa.

Aliongeza kuwa iwapo ukuruba kati ya Kenya Kwanza na ODM utaendelea, basi kuna uwezekano wa Rais Ruto kupata kura nyingi eneo la Pwani mwaka 2027.Hata hivyo, akiwa Taita Taveta, Dkt Ruto alipuuza dhana kwamba anafanya kampeni akikashifu wapinzani wake kwa kushiriki kampeni za mapema za kura za 2027.

Katika Kaunti ya Kilifi, kwa mara nyingine alisisitiza kuwa ziara yake haikuwa ya kisiasa bali ya kushirikiana na wawekezaji.

“Sipo hapa kwa sababu nyingine bali ni kwa nia ya kuungana na wananchi na viongozi wa Kilifi katika mkutano huu adhimu wa uwekezaji utakaowapa wawekezaji kutoka sehemu zote za Kenya, Afrika na dunia kwa jumla nafasi ya kuwekeza. katika Kaunti ya Kilifi wanapotafuta fursa hapa, pia watapata fursa ya kuwekeza kote katika Kenya,” akasema.

Tangu kuundwa kwa Serikali Jumuishi, viongozi wa ODM wamejitokeza hadharani kumuunga mkono Rais Ruto.Katika ziara zake zote katika ngome za ODM kufikia sasa, Rais na washirika wake wamekuwa wakisisitiza umoja wa kitaifa na mgao sawa wa rasilimali za kitaifa.

Rasilmali

Hili linaonekana kama shambulio la wazi dhidi ya Bw Gachagua ambaye, kabla ya kuondolewa kwake madarakani, aliwahimiza wafuasi wake kuunga mkono siasa za kimaeneo na usambazaji wa rasilimali kulingana na idadi ya watu.

Mchanganuzi wa siasa, Kauli Mwatela anasema ziara za mara kwa mara za Rais eneo la Pwani ni za kimkakati kwani huenda analenga kura nyingi zaidi 2027 kuliko alizopata katika uchaguzi wa 2022.Mnamo 2022, Bw Odinga alidumisha umaarufu wake katika eneo hilo kwa kuzoa kura 649,913 katika kaunti sita, huku Dkt Ruto akipata 336,478, kulingana na data kutoka kwa Tume ya Uchaguzi (IEBC).

Licha ya Rais kupata uungwaji wa wazi kutoka kwa viongozi wanaoegemea upande wa ODM, kila anapozuru nchi, baadhi ya wanachama wa ODM wamekuwa wakisisitiza kuwa chama hicho kitasimamisha mgombeaji wake wa urais 2027.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*