Ruto apiga densi ya Kasongo huku hasira za Gen Z zitanda – Taifa Leo


HATUA ya Rais William Ruto ya kukumbatia lakabu yoyote kwa kejeli na kupuuza hasira za raia imetajwa kuwa hatari huku vijana wakipanga kuendelea kuandamana kushinikiza wenzao waliotekwa nyara waachiliwe.

Katika siasa, Rais Ruto amedhihirisha kuwa mtu anayeishi kwa falsafa ya kutengeneza juisi kutoka kwa ndimu alizokabidhiwa. Kwa hivyo, alivyoitwa Kasongo, kurejelea jina la wimbo ambao pia umehusishwa na ujanja, Rais alisakata densi ya wimbo huo hadharani.

Mkesha wa Mwaka Mpya, waliohudhuria hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Dkt Ruto katika Ikulu ndogo ya Kisii waliachwa katika mchanganyiko wa hisia wakati Deejay alipocheza wimbo uliofufuliwa majuzi ulioimbwa 1977, Kasongo, mara tu Rais alipokuwa akiondoka.

Jina la wimbo wa Kasongo

Wanamtandao wamekuwa wakitumia jina la wimbo huo uliovuma kumrejelea Rais,Kinyume na matarajio ya wengi, Rais alicheza densi wimbo huo wa Orch Super Mazembe, ambao unahusu mwanamke akimtaka mumewe, Kasongo, arejee nyumbani ulipochezwa.

Umati ulisisimka huku Dkt Ruto, pamoja na Mkewe Rachael Ruto, wakicheza wimbo huo huku wakisalimia waliokuwa wamehudhuria chakula cha jioni.

Hata walinzi wake walionekana kufurahia wimbo huo huku wakihangaika kumkinga na wale waliojaribu kumkaribia.Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura, Waziri la Maji Eric Mugaa, Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga na Mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro walijumuika na Rais.

Haijabainika mara moja ikiwa Deejay aliagizwa na kikosi cha Rais kuucheza wimbo huo ili kutoa ujumbe kama vile alivyofanya na lakabu ‘Zakayo’.

Mazishi ya mamake Wetang’ula

Mnamo Ijumaa, wakati wa mazishi ya mamake Spika wa Bunge, Moses Wetang’ula, Rais kwa mara ya kwanza alizungumza kuhusu lakabu ya Kasongo kwa kejeli, pamoja na ‘Zakayo’ ambayo aliyoitwa kwa sababu ya sera zake za ushuru.

Kulingana naye, wapo watu ambao hawataki ajikite kwenye maendeleo na ndiyo maana “wanachochea” umma dhidi ya serikali.

“Kuna watu kwenye mitandao ya kijamii wanataka kuendelea kuchochea watu wakisema hakuna maendeleo na wananiita Kasongo na Zakayo. Kasongo sio mbaya, tuendelee nayo,” alisema Rais Ruto.

Awali, alikuwa amekumbatia Zakayo.“‘Zakayo’ pia si mbaya kwa sababu inazungumzia kukusanya ushuru wa kutosha ili kuendeleza Kenya mbele. Kwa hakika, Zakayo ndiye aliyetembelewa na Yesu. Kama wewe si Zakayo, Yesu atakutembeleaje?” aliuliza Rais.

Mara ya kwanza kutaja Zakayo

Haikuwa mara ya kwanza kutaja Zakayo. Mnamo Februari mwaka jana alipokuwa akizungumza katika hafla ya Mamlaka ya Mapato ya Kenya jijini Nairobi, aliwataka Wakenya kulipa ushuru ili kuendeleza nchi na kusema hajali anapewa jina gani kwa juhudi zake za kuongeza ukusanyaji wa ushuru.

“Sijali kuitwa Zakayo. Lazima tuendeleze nchi yetu kwa kodi zetu wenyewe. Nitafanya jambo linalofaa kwa nchi bila kujali majina ninayoitwa, ikiwa ni pamoja na Zakayo,” Rais Ruto alisema.

Na alipoteua mawaziri ‘wataalamu’ kutoka ODM ya Bw Raila Odinga, alisema angalau hataitwa Zakayo peke yake.Mtaalamu wa mikakati na uongozi Auscar Odhiambo Wambiya alisema kwa kukumbatia lakabu zake, Rais anaonyesha weledi wa mwanasiasa.

Anacheka na kukumbatia lakabu

Alibainisha kuwa Dkt Ruto ni mzuri katika hili; kwamba, anacheka kukosolewa na kumbatia lakabu.

“Hii inaonyesha tu kwamba anavumilia wakosoaji wake. Ni mbinu ya kisiasa ambayo anafaa kusifiwa kwani anatumia ndimu alizotupwa kutengeneza juisi,” akasema Bw Wambiya, mshauri wa mikakati katika kampuni ya Milestones Consultants.

 

Waandamanaji wakifunga barabara ya Expressway eneo la Mlolongo, Nairobi. Picha|Boniface Bogita

Hata hivyo, alitumai kuwa Rais hafanyi hivyo mchana tu na kuwafuata wakosoaji wake nyakati za usiku kupitia utekaji nyara.Baadhi ya wachanganuzi wanahisi kwamba, kwa Rais kukumbatia na kuchezea lakabu alizopewa— anapuuza masuala mazito.Vijana ambao wamempa lakabu hizo, wanapanga kuandamana leo kushinikiza wenzao waliotekwa nyara kuachiliwa.

Mtaalamu wa masuala ya mawasiliano Odhiambo Otieno alisema kwamba hatua ya Rais Ruto haiondoi hasira miongoni mwa Wakenya.Mtangazaji wa redio Oga Obinna amekasirishwa na wanasiasa wanaomzunguka Dkt Ruto na kumtetea ili kumfurahisha.

Amekalia bomu la muda

“Mheshimiwa Rais, umekalia bomu la muda kwa sababu vijana wana hasira na njaa. Sielewi kwa nini watu wako wa karibu hawakuambii ukweli. Mambo ni mabaya. Zungumza na vijana na uwasikilize,” alisema Obinna.

Kwake, kuwaleta washirika wa Bw Raila Odinga katika utawala wake hakuwezi kubadilisha hasira, njaa na kutamauka kwa baadhi ya Wakenya ambao wanahisi kutoridhishwa na utawala wa Kenya Kwanza, hasa kuhusu utekaji nyara wa hivi majuzi wa wakosoaji wa serikali.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*