RAIS William Ruto ametetea vikali hatua ya serikali yake kuongeza ushuru (VAT) kwa bidhaa muhimu za kimsingi, akisema hilo linalenga kuboresha uchumi wa Kenya.
Akihutubu wakati wa maadhimisho ya Jamhuri 2024, Alhamisi, Desemba 12, katika Bustani ya Uhuru, Nairobi, Rais aliwataka Wakenya kuwa ‘wavumilivu’ akihoji matunda ya maamuzi yake yatakuwa matamu baadaye.
Dkt Ruto alisema shabaha ya serikali ya Kenya Kwanza ni kuona uchumi unaimarika na maisha yanakuwa rahisi.
“Kwa kuufanya uchumi uwe bora, hatuna budi ila kukaza mshipi,” alisema.
Rais Ruto aliongoza taifa kuadhimisha miaka 61 ya Kenya kupata uhuru wa kujitawala kama Jamhuri, ambapo alitumia jukwaa hilo kuainisha miradi ya maendeleo aliyofanya kipindi cha miaka miwili ofisini.
Tangu achukue hatamu za uongozi 2022, utawala wa Ruto umekuwa ukikosolewa na kunyooshewa kidole cha lawama kwa kuongeza ushuru na ada kiholela.
Aidha, aliongeza ushuru wa mafuta ya petroli kutoka asilimia nane iliyowekwa na mtangulizi wake, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, hadi asilimia 16.
Mafuta ya petroli, bei inapopanda huathiri bidhaa muhimu za kimsingi kama vile chakula.
Rais, hata hivyo, wakati wa maadhimisho ya Jamhuri 2024, alisema hatua ambazo Wizara ya Fedha imechukua, “anaona taifa limeanza kukua”.
Alitaja uzinduzi wa bima tata ya afya ya SHIF, kuajiriwa kwa zaidi ya walimu 50, 000 tangu atwae uongozi, kati ya sera na maendeleo Kenya Kwanza inajivunia.
“Maendeleo yakija, kuna wanaoyaunga mkono na wengine wanayapinga…” Rais alisisitiza.
Ruto alihoji anaposema bei ya bidhaa muhimu za kimsingi imeshuka, anaashiria ukweli wa mambo.
Mwaka huu, Juni, taifa lilishuhudia maandamano yaliyoongozwa na vijana wa Gen Z kupinga kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2024, na gharama ya maisha kuwa ghali.
Leave a Reply