HATIMAYE Rais William Ruto amewateua wanachama wa jopo litakaloendesha mchakato wa uteuzi wa mwenyekiti na makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Kupitia chapisho maalum la gazeti rasmi la serikali toleo la Januari 27, 2025, Dkt Ruto aliwateua wafuatao kuwa wanachama wa jopo hilo; Fatuma Saman, Dkt Nelson Makanda, Balozi Koki Muli, Profesa Adams Oloo, Evans Misati, Nicholas Bore Kipchirchir, Andrew Tanui Kipkoech, Carolene Kituku na Linda Kiome Gakii.
Tisa hao wameapishwa na Jaji Mkuu Martha Koome kuanza kazi rasmi.
Rais amefanya uteuzi huo siku tatu baada ya Mahakama ya Kiambu kutupilia mbali kesi zilizowasilishwa mbele yake kupinga uteuzi wa jopo hilo.
Jaji wa mahakama hiyo Dola Chepkwony alifutilia mbali kesi ya kwanza iliyowasilishwa na Bonface Njogu akidai watu wanaoishi na ulemavu hawajajumuishwa kwenye orodha ya watu waliopendekezwa kwa uteuzi.
Jaji huyo pia alizima kesi iliyopinga utaratibu uliotumia kuteua mwakilishi wa muungano wa Azimio katika jopo, akisema madai kuwa uteuzi huo haukufanywa kwa njia ya ushindani “hayakufafanuliwa”.
Rais Ruto pia ameteua wanachama hao tisa wa jopo la kuteua makamishna wa IEBC siku moja baada ya kuwekewa presha na viongozi wa upinzani wakiongozwa na Kalonzo Musyoka, wakisema kujivuta kwake kunaweza kulitumbukiza taifa hili katika mzozo wa kikatiba.
“Ikiwa kufikia Jumatatu (Januari 27, 2025) Ruto hatakuwa ameteua wanachama wa jopo la kuteua makamishana wa IEBC tutatoa taarifa kamili kuhusu suala hilo. Kesi imeondolewa na sasa hana sababu ya kutoteua wanachama wa jopo hili ili lianze kuteua makamishna wapya wa tume hii,” Bw Kalonzo akasema Januari 26, 2025 baada ya kuhudhuria ibada ya Jumapili katika kanisa moja eneo bunge la Dagoretti Kaskazini.
Wengine waliotoa makataa kwa Rais Ruto kuhusu suala hilo ni Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiahi Kioni, Kiongozi wa chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) Eugene Wamalwa na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna.
Mchakato wa uteuzi wa makamishna wa IEBC ulikwama mnamo Julai 2023, baada ya serikali kuagiza jopo la zamani lililoongozwa na Dkt Makanda kusitisha shughuli hiyo ili kutoa nafasi kwa Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (Nadco) kutoa mwelekeo kuhusu suala hilo.
Hii ni baada ya mrengo wa Azimio ulioongozwa na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kudai Rais Ruto aliteua jopo hilo, kivyake, bila kufanya mashauriano na wadau wengine.
Baadaye mnamo Novemba 23, 2023, kamati ya Nadco iliyoongozwa na Bw Musyoka na kiongozi wa wengi Kimani Ichung’wah ilipendekeza kuwa jopo hilo la watu saba livunjwe na lingine lenye wanachama tisa liundwe.
Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya IEBC ya 2024, uliolenga kufanikisha utekelezaji wa pendekezo hilo, ulipitishwa katika Bunge la Kitaifa na Seneti mnamo Julai 14, 2024 na ukatiwa saini na Rais Ruto wiki moja baadaye.
Hapo ndipo mvutano mwingine kuhusu uanachama wa jopo hilo jipya ulioanza na hatimaye ukafikishwa Mahakamani.
IEBC imesalia bila mwenyekiti na makamishna kuanzia Januari 17, 2023, pale mwenyekiti wa zamani Wafula Chebukati na makamishna Boya Molu na Profesa Abdi Guliye walipoondoka afisini baada ya kukamilisha muhula wao wa miaka sita.
Awali, mnamo Desemba 2022, makamishna wanne; aliyekuwa naibu mwenyekiti Juliana Cherera, Justus Nyang’aya na Francis Wanderi walilazimishwa kujiuzulu.
Hii ni baada ya wao kulaumiwa kutishia kusababisha ghasia nchini kwa kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais yaliyotangazwa na Bw Chebukati Agosti 15, 2022 katika ukumbi wa Bomas of Kenya.
Naye Bi Irene Masit aliyedinda kujiuzulu wakati huo alipigwa kalamu mapema Januari 2023, kufuati pendekezo la jopo lililoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa Aggrey Muchelule.
Jopo hilo lililochunguza mienendo yake kwa siku 15 lilimpata Bi Masit na hatia ya kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa Rais Ruto ushindi “kinyume cha taratibu za kisheria.”
Kwa hivyo, tangu Januari 17, 2023, IEBC imesalia bila mwenyekiti na makamishna na kulemazwa kiasi cha kutoweza kuendesha chaguzi ndogo wala kuanza mchakato wa kuanisha upya mipaka ya maeneo wakilishi.
Kufikia sasa maeneo bunge ya Banisa, Ugunja na Magarini hayana wabunge. Eneo bunge la Banisa lilisalia wazi kufuatia kifo cha Kullow Hassan mnamo Machi 23, 2024.
Eneo bunge la Ugunja lilibaki bila mwakilishi mnamo Julai 14, 2024 baada ya kuteuliwa kwa James Opiyo Wandayi kuwa Waziri wa Kawi huku lile la Magarini likisalia wazi baada ya mahakama kubatilisha ushindi wa Harisson Garama Kombe katika uchaguzi wa 2022.
Isitoshe, zaidi ya wadi tisa nchini hazina wawakilisha baada ya madiwani kufa na wengine ushindi wao kubatilishwa.
Leave a Reply