Sababu iliyofanya bonasi za majani chai kukosa ladha mwaka huu – Taifa Leo


MAENEO yanayokuza majani chai kwa wingi yameathirika pakubwa huku kiwango cha bonasi inayotolewa na Shirika la Maendeleo ya Wakulima wa Majani Chai Nchini (KTDA) kikizidi kudorora.

Huku msimu wa marupurupu ukiwadia, ambao kwa kawaida huandamana na mbwembwe na starehe za kila aina kutokana na wingi wa hela, kimya kimetanda katika kaunti za Kericho, Bomet, Embu, Murang’a, Meru, Nandi, Kiambu na Nyeri huku wafanyabiashara wakishindwa la kufanya.

Kinyume na hapo awali ambapo msimu huu hufurika pesa, wauzaji duka na vituo vya pombe wanashuhudia wateja wachache huku waendeshaji bodaboda wakilalamikia hela kupungua na barabara zilizotulia.

Kaunti takriban 21 ambazo husubiri kwa hamu msimu wa marupurupu kila mwaka sasa zimepoteza mvuto wake huku marupurupu ya majani chai yakizidi kupungua kila mwaka.

Marupurupu ya mwaka uliopita

Mwaka uliopita, 2023, wakuzaji majani chai walilipwa marupurupu ya Sh44.15 bilioni ikilinganishwa na Sh62.88 bilioni 2022.

Hata hivyo, kiasi cha jumla hakijabainishwa kwa viwanda vyote 71 vya majani chai vinavyojumuisha 54 vilivyosajiliwa na 17 viungani.

“Inatarajiwa kuwa kiasi chote kitatangazwa katika mkutano mkuu (AGM) ujao unaofanyika kila mwaka kwa wakurugenzi wote wa KTDA,” msimamizi mmoja wa KTDA alieleza Taifa Leo, Alhamisi.

Mwaka wa 2023, wakulima wa majani chai walichangia Sh140 bilioni kwa uchumi kutokana na bidhaa za majani chai zilizouzwa katika mataifa ya kigeni ikilinganishwa na Sh138 bilioni (2022) na Sh136 bilioni (2021).

Kwa wakulima wengi, mabilioni hayo hana maana kubwa ikiwa hayawafaidi kiuchumi.

Sekta hiyo inajumuisha wakulima 680,000 wa mashamba madogo madogo ya majani chai wanaopeleka mazao yao kwa viwanda vya KTDA nchini.

Wanawake wakifanya kazi ya kuchuma majanichai. Bonasi ya zao hili imepungua mno mwaka huu jambo lililoondoa msisimko uliohusishwa na msimu wake. Picha|Maktaba

“Siku zimeisha ambapo wanawake waliojikwatua kwa mavazi ya kuvutia wangehamia katika miji inayokuza majani chai wakiwalenga wakulima msimu huu. Kulemazwa kifedha miongoni mwa wakulima kutokana na sababu kadhaa kumebadilisha mambo kabisa katika kanda za kukuza majani chai huku msimu wa marupurupu ukifungwa ghafla,” anasema mfanyabiashara kutoka Murang’a, Edwin Mwai.

Mkulima kwa jina Wilson Sigei kutoka Bomet alisema hajagundua wala kuhisi kuwa ni msimu wa bonasi kwa sasa.

Janet*, ambaye ni mchuuzi wa ngono mjini Kericho, anasema kwa miongo miwili ambayo amefanya kazi hiyo, hajawahi kuona msimu ulio chini jinsi hii.

“Wakulima wa majani chai hawatumii hela kama walivyokuwa wakifanya. Wengi sasa huenda vituo vya pombe duni au kujiepusha kunywa kabisa,” anasema.

Bi Mary Nyambura, ambaye ni mkulima mjini Meru anayepeleka majani chai yake katika kiwanda cha majani chai cha Githongo anasema wanawake wengi sasa wanahusika zaidi katika usimamizi wa hela nyumbani.

“Kinyume na hapo mbeleni wakati mabwana walidhibiti jinsi pesa zinavyotumiwa, wanawake sasa wanahakikisha zinatumiwa kwa busara. Pesa hutumiwa kwa njia bora sio kiholela,” anafafanua.

Imetafsiriwa na Mary Wangari



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*