WABUNGE wawili na magavana wawili wa zamani ni kati ya maafisa, wanafamilia na wandani ambao wanaandamwa na Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi (EACC) kuhusu wizi wa mamilioni ya pesa.
EACC kwenye ripoti yake ya robo mwaka kati ya Julai na Septemba 2024 imewashutumu maafisa hao wa ngazi ya juu kwa kushiriki ufisadi. Ripoti hiyo ilichapishwa mnamo Jumamosi.
Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Uasin Gishu Gladys Boss Shollei na mwenzake wa Bungoma Catherine Wambilianga pamoja na waliokuwa magavana Mohamed Mohamoud (Wajir) na Alex Tolgos (Elgeyo Marakwet) ni kati ya wale ambao watashtakiwa kutokana na ufisadi.
EACC inamtaka Bi Shollei ashtakiwe kwa kukiuka kanuni za utoaji tenda wakati wa kununua samani kwa afisi ya Jaji Mkuu. Bi Shollei ambaye alikuwa msajili wa mahakama wakati huo alifikishwa katika mahakama ya Milimani kuhusiana na suala hilo la ukiukaji wa kanuni za tenda.
Hata hivyo kesi hiyo ilipndolewa kwa kuwa ilikuwa ikihitilafiana na nyingine iliyokuwa ikiendelea na sasa imefufuliwa akidaiwa kushiriki ufisadi.
Pia anaandamwa na kesi nyingine ambapo ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za serikali zilionyesha kuwa idara ya mahakama ililipa Sh46.45 milioni kwa Kampuni ya Ms Timsales ili kujenga Mahakama ya Mavoko ilhali haikufanya kazi hiyo.
Bi Wambilianga naye anakabiliwa na madai ya kutumia Sh329,578 kila mwezi, pesa za afisi yake kuwalipia wanawe ada ya bima katika kampuni ya Bima ya Britam.
Kwa jumla alitumia Sh5.49 milioni kujilipia pamoja na wanawe wawili ada hizo za bima ya maisha. Pia anaandamwa kwa kushirikiana na wafanyakazi katika afisi yake kupanga njama ya kuiba pesa ambazo ni Sh20.1 milioni.
Bw Tolgos naye amejpata baya kutokana na malipo ya zaidi ya Sh1.75 bilioni ambazo zililipwa kwa kampuni inayohusishwa naye na mshirika wake kati ya 2013-2016 wakati ambapo alikuwa afisini.
Kampuni hiyo ya mafuta ya Kobcom iliwasilisha mafuta kwa kaunti ilhali haikutuma maombi yoyote ya tenda.
Bw Mohamoud, mkewe na mwanawe pamoja na wakurugenzi wa kampuni 12 wanaandamwa kutokana na Sh902.8 milioni ambazo zililipwa kampuni hizo 12 kati ya 2018-2021.
Leave a Reply