IWAPO wewe ni mgeni katika Kaunti ya Lamu, huenda ukachanganyikiwa na kukosa kutofautisha baina ya misikiti na hospitali.
Aghalabu utaishia kudhani kwamba waja wanaoingia hospitalini kutibiwa si wagonjwa ila ni waumini wa dini ya Kiislamu wanaoenda kuswali misikitini.
Hili linatokana na kwamba majengo ya hospitali karibu zote kuu za kaunti hiyo yametengenezwa kwa kutumia ramani inayoshabihiana na ile ya misikiti.
Hospitali kuu za Lamu kama vile ile ya King Fahd iliyoko kisiwani Lamu, Faza iliyoko Lamu Mashariki, Mpeketoni iliyoko Lamu Magharibi, Mokowe na Witu, zote majengo yake yanaoana na yale ya msikiti.
Mbali na hospitali, majengo mengine mbalimbali pia yamechukua muundo huu. Baadhi ni vituo kama vile kile cha kuokoa waliodhulumiwa kingono na kijinsia (SGBV) mjini Mokowe na kile cha matibabu ya waraibu wa dawa za kulevya cha Methadone (MAT) kilichoko kisiwani Lamu.
Taifa Leo ilizama ndani kutaka kujua sababu za majengo mengi katika Kaunti ya Lamu, zikiwemo hospitali, zahanati na vituo vingine yakajengwa kwa muundo wa misikiti.
Kwa mujibu wa Afisa Mkuu Msimamizi wa Idara ya Mipango na Miundomsingi Katika Serikali ya Kaunti ya Lamu, Alex Jimbi Katana, maamuzi hayo yanatokana na kwamba Lamu ni eneo linalotambulika kwa kuwa kitovu cha dini ya Kiislamu.
Bw Jimbi anasema ni kutokana na hali hiyo ambapo ramani nyingi za majengo yanayoezekwa, iwe ni kisiwani Lamu au sehemu nyingine za kaunti hiyo zinazingatia sana muonekano wa msikiti. Kulingana naye, majengo ya namna hiyo yameweza kutoa taswira kamili ya jadi kuihusu Lamu na historia yake.
“Lamu, hasa Mji wa Kale, ndio kitovu cha Uislamu katika Ukanda wa Afrika Mashariki. Ni mji uliodumu kwa zaidi ya miaka 700. Majengo mengi hapa, zikiwemo hospitali, yamezingatia sana ramani yenye muonekano sawa na msikiti.
“Hilo limesaidia kuhifadhi muonekano asilia wa eneo hili ambalo Uislamu ndiyo dini iliyokita mizizi. Lamu yenyewe iko na misikiti mingi ipatikanayo kwenye maeneo au mitaa mbalimbali,” akasema Bw Jimbi.
Anataja hatua ya Lamu kupandishwa hadhi na Shirika la Umoja wa Mataifa Kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) mnamo 2001 kama mojawapo ya maeneo yanayotambuliwa ulimwenguni kwa kuhifadhi ukale na tamaduni zake kuwa miongoni mwa sababu kuu zinazosukuma majengo mengi kudumishiwa muundo wa misikiti.
Afisa huyo anataja Ramani za Jadi za Ujenzi, Utamaduni na Biashara kuwa masuala matatu makuu yaliyosababisha Lamu kutambuliwa na kupewa hadhi ya eneo la ukale na UNESCO.
“Idara yangu imejitahidi kuhakikisha wanaojenga nyumba leo hii pia wanapokea idhini ya ni ramani gani zitapasishwa ili wakubaliwe kujenga.
“Lazima ramani zote zilingane na sheria zilizopo kabla ya ujenzi kutekelezwa. Tumehakikisha kuna ulinganifu wa majumba ya zamani na sasa, ambapo mengi ya majengo hayo yanaoana na msikiti,” akasema Bw Jimbi.
Waziri wa Afya, Kaunti ya Lamu, Dkt Mbarak Bahjaj pia alitaja historia, tamaduni, dini na hadhi iliyopewa Lamu na UNESCO kuwa sababu zinazochangia miundo ya majengio mengi kufanana na yale ya kale ambayo ni sawa na msikiti.
Bw Bahjaj anasema ni kupitia majengo hayo ambapo hadhi ya Lamu inazidi kuhifadhiwa na kuendelezwa.
“Watu wasisikie vibaya kuona hata hospitali zetu zikiwa na majengo sawa na misikiti. Lamu ni mji wa kihistoria ambao una tamaduni na uasilia wake.
“Isitoshe, majengo yanayojengwa kwa muundo wa misikiti ni kumaanisha ni katika harakati za kuoanisha Lamu ya jadi na sasa ili ukale usiangamie,” akasema Bw Bahjaj.
Wakazi hata hivyo walipongeza miundo ya majengo yanayofanana na misikiti Lamu, wakishikilia kuwa ni kupitia majengo hayo ambapo fahari ya Lamu hutambuliwa kiurahisi. Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Lamu, Mbwana Shee, alisema endapo watu wataruhusiwa kujijengea nyumba zao vivi hivi, hadhi na taswira ya Lamu itaangamia kabisa.
“Majengo ya zamani yanayoshabihiana na misikiti ndiyo fahari yetu kama watu wa Lamu. Yaani ni rahisi kwa anayeingia Lamu kujua wazi kwamba watu wa Lamu ni wa dini gani.
“Lamu ni eneo lililotawaliwa na Waarabu, hivyo kuleta kizazi cha Waswahili ambao dini yao ni Uislamu. Napongeza kuendelezwa mwa majengo hayo ya zamani. Ndiyo fahari yetu,” akasema Bw Shee.
Bi Raya Famau, ambaye ni Afisa Mtendaji wa Shirika la Wanawake la Lamu Women Alliance, pia alipongeza msimamo wa kaunti kuendeleza majengo yenye muonekano sawa na misikiti, akishikilia kuwa ni kupitia maamuzi hayo ambapo tamaduni na ukale wa Lamu unaendelezwa.
Afisa wa Halmashauri ya Makavazi na Turathi za Kitaifa nchini (NMK) wa Kaunti ya Lamu, Mohammed Mwenje, hata hivyo alieleza wasiwasi wake kwamba huenda maarifa au ufundi wa ujenzi wa majengo ya zamani ukaangamia endapo hatua mwafaka hazitachukuliwa kupitisha ujuzi huo kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Bw Mwenje alilalamika kuwa wazee wengi wenye maarifa ya ujenzi wa jadi kwa sasa wamestaafu huku wengine wakifariki.
“Leo hii hatuna mafundi tena wa kutujengea hizi nyumba za jadi. Vijana nao wamekuwa wakisusia kujifunza ujuzi huo na kuuendeleza.
“Ipo haja ya fedha kutengwa ili kuendeleza hamasa na mafunzo kwa vijana kupokezwa ujuzi huo na kuuendeleza ili kuzuia usiangamie katika miaka ijayo,” akasema Bw Mwenje.
Leave a Reply