WAKAZI zaidi ya 1,000 wa Visiwa vya Manda, Kaunti ya Lamu wanaomba warudishiwe mashamba yao wanayodai yamenyakuliwa na mabwanyenye.
Inadaiwa walipokonywa mashamba hayo na wawekezaji ambao walishirikiana na maafisa katika wizara ya ardhi na mawakili.
Sasa, mahakama imeamuru kesi hiyo isikizwe Desemba 18,2024.
Jaji Bahati Mwamuye aliwaamuru wawakilishi wa wakazi hao waliowasilisha kesi hiyo katika Mahakama ya Milimani wakabidhi washtakiwa nakala za kesi hiyo kabla ya saa 11 alasiri mnamo Alhamisi Novemba 28,2024.
Na wakati huo huo Jaji Mwamuye amewaagiza washtakiwa wawasilishe ushahidi wao Novemba 29,2024.
Jaji huyo alisema malalamishi ya wakazi hao yanafaa kusikizwa na kuamuliwa ikitiliwa maanani “haki ya kumiliki mashamba na mali ni suala nyeti.”
“Mahakama hii imezingatia kwamba ombi la kufutiliwa mbali kwa agizo linalowazuia polisi kuwakamata na kuwashtaki waliohusika na unyakuzi wa mashamba ya walalamishi linapaswa kuamuliwa,” alisema Jaji Mwamuye.
Jaji huyo aliongeza kusema pia kuna ombi la kufungwa kwa kesi iliyowasilishwa na Alex Githinji Njage katika Mahakama kuu ya Milimani na kurudishwa Mahakama kuu ya Malindi kuamuliwa uko.
Jaji Mwamuye aliamuru kesi hiyo isikizwe Desemba 17,2024.
Kupitia kwa Bi Fatuma Mahmoud na Wafiya Hussein wakazi hao wanadai haki zao kumiliki mali na ardhi zimehujumiwa na kunyanyaswa na Msajili wa ardhi katika afisi ya eneo la Lamu.
Vile vile wakazi hao wamelalama kwamba jitihada zao kushtaki wakili mmoja na msajili huyo wa ardhi zimegonga mwamba.
Walitaja kuwa wamepata maagizo kisiri kutoka Mahakama Kuu ya Milimani Nairobi kuwazima maafisa wa kukabili uhalifu kuwachunguza na kuwafungulia mashtaka.
Mahakama imeelezwa kwamba wakazi hao wamepigwa na butwaa kugundua kwamba ijapokuwa ni wao wana hatimiliki za mashamba yao, wizara ya ardhi imetoa vibali vingine vya umiliki wa mashamba yao kwa watu wengine ambao hawajawauzia ardhi yao.
Walalamishi hao wameeleza mahakama kuu Milimani kwamba “ni jambo la kustaajabisha kwamba wana hatimiliki ya mashamba yao lakini pia wizara ya ardhi imewapa watu wengine hati za mashamba yao.”
Wakazi hao wamesema mahakama kuu Malindi iliamuru kuwa wao ndio wamiliki halisi wa mashamba hayo na “hakuna mtu yeyote anafaa kudai umiliki kwa vile wao ndio wamiliki asili.”
Katika malalamishi kwa mahakama kuu kupitia mawakili Martina Swiga na Danstan Omari wakazi hao wamedai wanyakuzi wa mashamba yao wamewasilisha kesi kisiri na kupata maagizo ya kuzuia maafisa wa DCI kuwachunguza.
Pia wamepata maagizo ya kuzuia Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) asiwafungulie mashtaka kuhusiana na unyakuzi wa mashamba yao.
Wakazi hao wameomba mahakama kuu pia iwajumuishe katika kesi iliyowasilishwa na Alex Githinji Njage kwa lengo la kuwasilisha ushahidi kuwezesha mahakama kufikia uamuzi wenye busara.
Wakazi hao wameeleza mahakama kwamba wataipa mahakama kuu Nairobi ushahidi kamili kuhusu umiliki wa ardhi ya zaidi ekari 1,000 iliyo na thamani ya mabilioni ya pesa.
“Tunaomba mahakama hii itushirikishe katika kesi iliyoshtakiwa na Bw Njage ili tuipe mahakama ushahidi wa asili ndipo itoe uamuzi wa haki na ulioshamiri ukweli mtupu,” Fatuma Mahmoud amedokeza katika ushahidi aliowasilisha mahakamani.
Kupitia kwa mawakili Swiga na Omari, wakazi hao wamesikitika kupoteza ardhi yao kwa matapeli lakini wana imani mahakama kuu ya Nairobi itarejesha ardhi yao.
Awali, Mahakama Kuu ya Malindi ilikuwa imewatambua wakazi hao wa Manda kuwa wamiliki halisi wa mashamba yao lakini kukachipuka hatimiliki nyingine za wanyakuzi.
“Twaomba mahakama kuu iturehemu na kuturudishia ardhi yetu,” Mahmoud aliililia mahakama.
Wakazi hao wamedai kwamba afisa mmoja wa usajili wa ardhi na wakili walishtakiwa kwa ulaghai wa ardhi lakini wakaachiliwa na mahakama ikidai DPP hakuwasilisha ushahidi wa kutosha kuthibitisha kesi dhidi ya watalaam hao wa masuala ya sheria.
Leave a Reply