Sababu za KUPPET kukemea KNEC kwa kuzuia baadhi ya walimu kusahihisha KCSE – Taifa Leo


CHAMA cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kadri (KUPPET) tawi la Kisii kimekashifu hatua ya Baraza la Mitihani ya Kitaifa nchini (KNEC) kwa kuwazuia baadhi ya walimu waliokuwa wanajiandaa kusahihisha mitihani ya kitaifa ya shule za sekondari (KCSE) mwaka huu wasihusike na zoezi hilo.

Katibu Mtendaji wa KUPPET eneo la Kisii Joseph Abincha amedai kuwa agizo la KNEC linaenda kinyume na kanuni za kimataifa za leba.

Akizungumza katika hafla ya mazishi ya mmoja wa wanachama eneo la Bomachoge Borabu, Bw Abincha  aliomba Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba atathmini uamuzi wa KNEC.

“Kwamba kuna shule zinazoshukiwa kuhusika katika wizi wa mitihani, haiwezekani walimu waliokuwa nyumbani wakati wa mitihani waadhibiwe,” akasema Bw Abincha.

“Walimu hawa walikuwa wanangoja mwezi Desemba ufike ili waanze kusahihisha mitihani hiyo. Ninamwomba waziri wa elimu akabili KNEC na kubadilisha uamuzi huu,” akaongeza.

Baraza la mitihani lilichukua hatua hii inayoibua mzozo mkali na walimu baada ya shule wanakofunzia walimu hao huko Kisii kuripotiwa kuwa na visa vya udanganyifu katika mitihani iliyokamilika juma lililopita.

Makumi ya visa vya udanyanyifu wa mitihani viliripotiwa katika kipindi cha mwezi mmoja wa mitihani ya kila mwaka ya KCSE.

Mnamo Novemba 22, walimu wanne wa shule ya upili ya Bobamba iliyoko Gucha, Kaunti ya Kisii, walitiwa mbaroni kwa kuhusishwa na wizi.

Kabla ya hapo, walimu 13 walikamatwa kwa tuhuma sawia katika shule ya sekondari ya Nyamninia, Kaunti ndogo ya Gem-Yala mnamo Novemba 11 na kufikishwa kizimbani.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*