BAADA ya Uchaguzi Mkuu wa 2022 Gavana wa Meru Kawira Mwangaza waziri wa zamani wa Kilimo Peter Munya walikuwa washirika wa karibu wa kisiasa.
Sababu ni kwamba Bw Munya alimpigia debe Bi Mwangaza, kupitia mbunge wa Tigania Mashariki Mpuru Aburi aliyeendeleza kauli mbiu ya “Ngabana ni mama” (Gavana ni Mama).
Bw Munya alichelea kumuunga mkono Kiraitu Murungi, aliyekuwa akitetea kiti chake, na ambaye alikuwa katika mrengo wa Azimio la Umoja-One Kenya, kutokana na uhamasa kati yao.
Hatimaye Bw Murungi alishindwa vibaya na kushikilia nambati tatu, nyuma ya Bi Mwangaza na Mithika Linturi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) aliyeibuka nambari mbili.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Bw Murungi kushindwa uchaguzini tangu alipojiunga na mashindani ya kisiasa kwa mara ya kwanza mnamo 1992 alipochaguliwa kuwa Mbunge wa Imenti Kaskazini.
Lakini sasa ukuruba wa kisiasa kati ya Bw Munya na Bi Mwangaza haupo tena.
Chimbuko la tofauti zao za kisiasa halijulikani, isipokuwa na wandani wao wa karibu pekee.
Gavana Mwangaza alipokabiliwa na hoja ya kumwondoa afisini, siku 10 pekee baada ya kuingia uongozini, alielekeza kidole cha lawama kwa “watu fulani” aliodai waliwashawihi madiwani kupitisha hoja ya kumwondoa afisini mara mbili.
Hata hivyo, Seneti ilizima majaribio hayo mawili ya madiwani wa Meru kutaka kumwondoa afisini Bi Mwangaza.
Lakini mnamo Agosti mwaka jana, Gavana huyo hakuponea kwani maseneta waliidhinisha hoja ya kumwondoa afisini.
Wakati huu Bi Mwangaza yuko mahakamani akijaribu kubatilisha hatua hiyo ya Seneti.
Gavana huyo anatarajiwa kujua hatima yake mnamo Machi 14, mwaka huu Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi kuhusu kesi yake ya kupinga kutimuliwa kwake
Uamuzi huo, unaosubiriwa, ndio umechochea moto wa siasa katika kaunti ya Meru.
Mikutano ya kisiasa inafanyika katika kaunti za Meru na Nairobi kupanga mikaka ya kisiasa
Mabw Murungi, Munya na Linturi sasa wanashirikiana kupanga mikakati ya kumwangusha Bi Mwangaza katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Lakini wanasiasa hao pia wanasema kuwa uamuzi wa Mahakama kuhusu kesi ya Bi Mwangaza utaamua ikiwa wataendelea kushirikiana chini ya mwavuli wa chama cha UDA chake Rais William Ruto au waamue kujiunga na mrengo wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Wanasiasa hao watatu wanasema kuwa utawala wa Bi Mwangaza umerudisha kaunti ya Meru nyuma kimaendeleo kinyume na hali ilivyokuwa wakati Bw Munya na Murungi walihudumu kama magavana.
Wanasiasa hao wanadai kuwa badala ya Bi Mwangaza kutekeleza miradi ya maendeleo, ameelekeza juhudi zake katika mipango isiyo na maana huku akiwatunuku washirika wake.
Bw Murungi, Munya na Linturi, walifanya mkutano wao wa kwanza mnamo Februari 18, sasa chache baada ya kuhudhuria mkutano ulioitishwa na Naibu Rais Kithure Kindiki katika makazi yake rasmi mtaani Karen, Nairobi.
Leave a Reply