Sababu za Mwangaza kutaka korti ibatilishe uamuzi wa kumtimua – Taifa Leo


GAVANA wa Meru Kawira Mwangaza anataka jaji abatilishe uamuzi wa kumtimua ofisini akidai Bunge la Kaunti na Seneti zilikiuka agizo la Mahakama Kuu ya Meru lililozima mchakato wa kumuondoa madarakani.

Mawakili wa Mwangaza, Elisha Ongoya na Elias Mutuma walimweleza Jaji Bahati Mwamuye kwamba kuondolewa kwake ni kudharau haki.

Ongoya alisema seneti ilikaidi agizo lililotolewa na Mahakama Kuu ya Meru mnamo Julai 24 2024 kusitisha mchakato wa kumuondoa ofisini.

‘Mwangaza hakupaswa kuondolewa ofisini na bunge la kaunti na Seneti kwa sababu kulikuwa na amri ya mahakama ya kusitisha mchakato wowote wa kumtimua,’ Ongoya aliambia Jaji Mwamuye.

Mawakili hao walisema kutokana na kudharau agizo hilo la mahakama, maafisa wakuu wa bunge la kaunti ya Meru wiki jana walipatikana na hatia ya kudharau mahakama na kupigwa faini au watupwe gerezani kwa miezi sita.

Akirejelea uamuzi wa Jaji Edward Murithii wa Mahakama Kuu ya Meru, Ongoya alimweleza Jaji Mwamuye kwamba Spika wa Bunge la Kaunti ya Meru, Ayub Bundi Solomon, karani wa Bunge la Kaunti ya Meru Jacob Kirari na Zipporah Kinya, diwani aliyeteuliwa katika Bunge la Kaunti ambaye ni naibu Kiongozi wa wengi waliowasilisha ombi la kumng’atua madarakani walihukumiwa kufungwa jela miezi sita wakishindwa kulipa faini ya Sh 100, 000 kila mmoja kwa kukiuka agizo lililotolewa Julai 24 2024 na Jaji P. Kassan kuzuia mjadala wowote kuhusu kuondolewa ofisini kwa Mwangaza.

Ongoya alimweleza Jaji Mwamuye kwamba ili kushinda haki madiwani kupitia Kinya waliondoa hoja ya awali ambayo mahakama ilikataza na kuwasilisha mpya, ambayo ilisababisha kuondolewa kwa Mwangaza ambaye alichaguliwa kwa kura nyingi katika uchaguzi mkuu wa 2022.

‘Kukiwa na agizo la mahakama, mchakato mzima wa kumtimua Mwangaza ni ubatili kisheria,’ alisema Ongoya.

Jaji alielezwa kwamba maseneta chini ya uongozi wa Spika Amason Kingi walipuuza agizo la mahakama la kuzuia kuondolewa kwa Bi Mwangaza

Ongoya aliwasilisha ushahidi unaoonyesha kuwa walifahamisha Seneti kuwepo kwa agizo la mahakama kusimamisha zoezi hilo.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*