Sababu za Rais Ruto kuhofia kutimua wandani wa Rigy G wanaoshikilia viti bungeni – Taifa Leo


MASWALI yameibuliwa baada ya mrengo wa Kenya Kwanza kusitisha mpango wa kuwaondoa wandani wa aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua kutoka nyadhifa za uongozi wa baadhi kamati za Bunge la Kitaifa na Seneti.

Duru zimeiambia safu hii kwamba hatua hiyo imeahirishwa baada ya Rais William Ruto kuingiwa na hofu kwamba hatua hiyo ingempotezea umaarufu zaidi sio tu katika Mlima Kenya bali maeneo mengine ya nchini.

Aidha, mpasuko ndani ya ODM kuhusiana na ukuruba kati ya Rais Ruto na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga unasemekana kuwa sababu nyingine ilichangia kupigwa breki kwa hatua ya kutimuliwa kwa wandani wa Gachagua wanaoshikilia nyadhifa za uongozi wa kamati mbalimbali.

Awali, mabadiliko hayo yalitarajiwa kufanywa kabla ya Bunge la Kitaifa na Seneti kuahirisha vikao vya kwa likizo ya ndefu ya Krismasi na Mwaka Mpya.

Lakini kufikia Alhamisi, Bunge la Kitaifa lilipoahirisha vikao vyake vya kawaida hati Februari 11, 2025, shoka halikuwa limewaangukia wabunge wandani wa Gachagua waliopinga hoja ya kumtimua afisi Oktoba mwaka huu.

Hata hivyo, wiki moja iliyopita, Seneta wa Laikipia John Kinyua, ambaye ni mwandani wa Gachagua, alijiuzulu wadhifa wake kama mwanachama wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC).

Nafasi yake ilitunukiwa Seneta wa Nyeri Wahome Wamatinga huku duru zikisema kuwa huenda alilazimishwa kung’atuka Kiongozi wa Wengi Kimani Ichungwa, hata hivyo, sasa anasema kuwa mabadiliko hayo hayakulenga wabunge ambao walipinga hoja ya kutimuliwa kwa Gachagua bali wenyekiti wa kamati za bunge ambao wamekuwa watepetevu katika majukumu yao.

“Wale waliokuwa wakilengwa ni wenyeviti na manaibu wenyeviti ambao wamekuwa wakikwepa majukumu yao. Malalamishi yametolewa na wanachama wa kamati husika na hata Spika mwenyewe kwamba kuna wenyeviti huwa hawahudhurii vikao vya kamati na hata vile vya kamati ya bunge,” akasema, akikana madai kuwa walengwa walikuwa wandani wa Gachagua pekee.

Naye Kiongozi wa Wachache Junet Mohamed alithibitisha kuwa kuwa mabadiliko hayo yalisitishwa hadi bunge la kitaifa litakaporejelea vikao vyake hapo mwaka.

“Tumesitisha mpango huo wakati huu. Hatukutaka watu fulani kuenda likizo wakiwa na nuksi. Sasa tutalishughulikia suala hilo baada ya wabunge kurejelea vikao vya kawaida Februari 11, 2024,” mbunge huyo wa Suna Mashariki akaeleza.

Lakini Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya alisema mipango ya kuwatimua ilisitishwa baada ya Rais Ruto kung’amua kuwa hatua hiyo ingemgharimu pakubwa kisiasa.

“Nadhani Rais wetu ameng’amua kuwa masuala muhimu ambayo anapaswa kushughulikia ni changamoto zinazokumba utekelezaji wa Bima ya SHIF, shida zinazokumba sekta ya elimu miongoni mwa masuala mengine wala sio sisi ambao tumeamua kusimama na Gachagua,” anaeleza.

Bw Gakuya, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa, ni miongozi mwa wabunge 44 waliopinga hoja ya kumtimua Gachagua.Mwingine ambaye angeangukiwa na shoka ni Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Usimamizi wa Utekelezaji wa Katiba (CIOC).

Aidha, Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti angetimuliwa kwa kukwepa kupiga kura kwa hoja ya kumtimua Bw Gachagua mnamo Oktoba 8, 2024.

Katika Seneti wale ambao wangeathiriwa na mabadiliko hayo ni; Seneta wa Kiambu Karungo Thang’wa ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Barabara, Seneta wa Kirinyaga Kamau Murango (mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo), Joe Nyutu (Elimu) na Seneta wa Nyandarua John Methu ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya Ardhi.

Afisa mmoja mwenye cheo cha juu serikalini wiki hii alinukuliwa akisema kuwa haja kubwa ya Rais Ruto wakati huu ni kuweka mikakati itakayorejesha imani ya Wakenya kwa serikali sio kuwakosesha matumaini.

“Kuwapokonya wandani wa Gachagua nyadhifa wanazoshikilia katika Bunge la Kitaifa na Seneti ni mojawapo wa hatua ambazo zitaigharimu serikali badala ya kuipa umaarufu,” afisa huyo akaeleza.Wabunge na maseneta wa ODM ni miongoni mwa wale ambao wangetunukiwa nyadhifa ambazo zingepokonywa wandani wa Bw Gachagua.

Lakini mgawanyiko unaoshuhudiwa katika chama hicho kuhusiana na fasiri ya uhusiano kati ya Bw Odinga na Rais Ruto.Huku kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohamed akitangaza wazi kuwa ataunga mkono sera za serikali kwa sababu zinafanana na zile za Azimio, katibu mkuu Edwin Sifuna anasisitiza ODM kama chama cha upinzani itaendelea kupinga sera hizo kama vile bima mpya ya kijamii (SHIF).



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*