SENETA wa Kaunti ya Kisii Richard Onyonka amekataa mwaliko wa kushiriki chakula cha jioni cha mkesha wa Mwaka Mpya kilichoandaliwa na Ikulu.
Katika taarifa kwa Vyombo vya Habari, Bw Onyonka alisema kuwa uamuzi wake unatokana na kushindwa kwa Serikali kuwaachilia vijana waliotekwa nyara ambao familia zao hazina utulivu na zinaendelea kuteseka kwa maumivu.
“Kwa sababu ya msimamo wangu wa dhati kuhusu masuala haya, sitahudhuria Sherehe ya Serikali ya Chakula cha Jioni kukaribisha Mwaka Mpya – katika Ikulu ndogo ya Kisii jioni ya Jumanne Desemba 31 2024, katika wadhifa wangu kama Seneta wa Kaunti ya Kisii. Hivyo basi, ninakataa mwaliko huo,’”alisema Bw Onyonka.
Mwanasiasa huyo wa upinzani, ambaye amekuwa akikashifu ufisadi serikalini, alisema kwamba hafurahishwi na wazo kwamba baadhi “yetu tutakuwa watu wa kawaida, wenye furaha na taadhima wakati familia zingine za Kenya zina maumivu. Alisema mwaka wa 2024 unaisha kwa hali duni sana kutokana na utekaji nyara unaoendelea wa vijana wa Kenya wanaomkosoa Rais Ruto na utawala wake.
“Utekaji nyara unaoendelea, ufisadi na ukiukaji wa haki za watu, hasa za vijana wa Kenya ni huzuni na uchungu kwa wengi. Inauma kukumbuka maisha yetu ya zamani. Ina maana kwamba Kenya inarudi kwenye enzi za giza; hakika, historia inajirudia,” ilisema sehemu ya taarifa yake Seneta Onyonka.
Alieleza kuwa Rais Ruto alipaswa kuwaachilia waliotekwa nyara kama ‘wito wake wa mwaka mpya wa umoja,na udugu wa Wakenya wote’.
Rais ameshikilia msimamo mgumu licha ya maombi ya Wakenya wa matabaka mbalimbali. “Wakenya wameuliza, wameomba na kumsihi Rais Ruto ambaye ameziba masikio yake!” alisema.
Alisema kiongozi wa nchi ameshindwa kuzingatia utawala wa sheria ambao aliapa kulinda. “Nina imani kubwa kwamba rais amekosa kutimiza kiapo chake ambacho anafaa kutii, kuhifadhi, kulinda na kutetea mamlaka, uadilifu na utu wa watu wa Kenya,” taarifa hiyo ilisema.
Katika taarifa hiyo, Bw Onyonka alisikitika kuwa mwaka wa 2024 umekuwa mwaka wa huzuni, misukosuko na uchungu kwa Wakenya huku serikali ikirudisha nyuma mafanikio ya demokrasia.Alisema kwamba Rais angekaribisha mwaka mpya kwa njia tofauti ya kurekebisha hali.
Shutuma za Bw Onyonka kwa serikali kunajiri siku moja baada ya Jaji Mkuu Mstaafu David Maraga alitoa taarifa kali akilaumu utawala wa Rais Ruto.Bw Maraga alitaja utawala wa Bw Ruto kuwa ‘usiojali’ kwa kukiuka mafanikio ya kikatiba ambayo nchi imepata kwa miaka mingi.Katika taarifa yake, Bw Maraga alisema kuwa mwaka wa 2025 utakuwa mwaka ambapo wakandamizaji watakabiliwa na haki.
Seneta huyo alikuwa miongoni mwa waliopinga dili za Adani ambazo hatimaye Rais Ruto alilazimika kuzifuta.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply