WAKENYA wangali wanalemewa na mzigo wa gharama ya maisha licha ya kushuka kwa bei ya bidhaa kama vile unga wa ngano, sukari na mafuta ya kupikia mwaka huu. Juhudi hizi zimekosa kuwapa Wakenya afueni ya gharama ya maisha, huku wengi wakilemewa na madeni kutoka na sera za ushuru za serikali.
Takwimu kutoka mashirika tofauti likiwemo Shirika la Kitaifa la Takwimu Kenya (KNBS), zinaonyesha imekuwa vigumu kwa Wakenya wengi mwaka huu kuweka chakula mezani na kukidhi mahitaji yao mengine.
Licha ya kushuka kwa bei za bidhaa katika kipindi hiki ikilinganishwa na mwaka jana, Wakenya bado wanalazimika kukabiliana na gharama ya juu ya maisha kutokana na kupungua kwa mapato kunakosababishwa na ushuru wa juu.
Hii ilifanya kupungua kwa kasi ya mfumuko wa bei mwaka huu kutozaa matunda. Mfumuko wa bei mwezi Desemba 2023 ulikuwa asilimia 6.8 ikilinganishwa na asilimia 2.8 ya sasa.
Uchanganuzi wa bei za bidhaa unaonyesha pakiti ya kilo mbili ya unga wa ngano, pakiti ya kilo mbili ya unga wa mahindi, na kilo ya sukari na mafuta viligharimu zaidi katika kipindi kama hicho mwaka jana.
Kilo moja ya viazi kwa sasa ni Sh26 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana. Pakiti ya kilo mbili ya unga wa ngano pia ni nafuu kwa Sh26, ikiuzwa kwa Sh169 huku kilo mbili za unga wa mahindi ikiuzwa Sh134 ikilinganishwa na Sh161 mwaka jana.
Petroli ambayo ilikuwa Sh217 lita katika kipindi kama hicho mwaka jana sasa ni Sh176 na dizeli pia imeshuka hadi Sh165.
Hata hivyo, kushuka kwa bei ya bidhaa hizi, kwa bahati mbaya, hakujapunguza mzigo kwa Wakenya ambao mapato yao yamepunguzwa kutokana na ushuru kama wa nyumba (AHL), makato ya Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni (NSSF), na Bima ya Afya ya Jamii (Shif).
Makato ya chini ya NSSF yalipanda kutoka Sh400 kwa mfanyakazi hadi Sh2,160 kwa mwezi. Shif inachukua asilimia 2.75 ya malipo ya jumla na Ushuru wa Nyumba unazoea asilimia 1.5.
Leave a Reply