WASANII kutoka Kaunti ya Nairobi walikumbukwa katika sikukuu ya Jamhuri Desemba 12, 2024 baada ya Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja kufichua kuwa barabara za jiji zitapewa majina yao.
Gavana huyo alisema serikali yake inalea vipaji vya vijana walio na talanta ya uimbaji huku wakiwatafutia soko.
“Tumeona sekta hii inakuwa, na Nairobi sasa inavutia wasanii wa ndani na wa nje. Tutakuwa tunawaheshimu wasanii hao kwa kupatia barabara majina yao,” alisema Gavana Sakaja.
Barabara hizo zitapewa majina ya wasanii baada ya gavana huyo kushirikisha wabunge wa Kaunti ya Nairobi.
“Kwa mfano kuna barabara moja katika mtaa wa South C itapewa jina la rapa Issah Mmari Wangui, anayejulikana zaidi kama E-Sir, ambaye kaka yake amekuwa miongoni mwa wale ambao wametutumbuiza,” aliongeza.
Rapa huyo ambaye alikuwa mzaliwa wa mtaa wa South C, alifariki Machi 16, 2003 akiwa na umri wa miaka 21 kutokana na ajali ya barabara akitoka Nakuru kurejea Jijini Nairobi.
Msanii huyo alianza kunoa makali kwenye sekta ya muziki mapema miaka ya 2000 na kutambuliwa na wengi kutokana na vibao maarufu vya “Hamunitishi,” “Mos Mos,”na “Boomba Train” (ambacho alimshirikisha mwanamuziki Nameless).
Leave a Reply