SAMAHANI, mwenzako naitambua danganya-toto mara moja ninapoiona! Hii ya Serikali ya Kenya kuwaahidi wananchi kwamba itawatafutia fursa 20,000 za kazi nje ya nchi kabla ya mwaka huu kuisha ni danganya-toto.
Mwaka umesalia wiki mbili na uishe.
Tangu lini Serikali ya Kenya ikatimiza wajibu wowote kwa kasi na umadhubuti huo? Hivi ina maslahi yapi katika shughuli hiyo ya Wakenya kuajiriwa nje ya nchi ikiwa si kuendeleza biashara ya utumwa, angaa ya kisasa, kwa nia ya kuvuna isikopanda?
Jambo linalozuga akili kupindukia ni kuwa sasa imeibuka kwamba ahadi ya Rais William Ruto kuwatafutia Wakenya kazi katika mataifa yanayojulikana kwa mishahara mizuri na mazingira rafiki ya kufanyia kazi si ya kweli.
Inavunja moyo mno unapojiandaa na kufika wanakofanyiwa usaili watu wanaotafuta kazi hizo, ukiwa na matumaini ya kwenda, mathalan, Australia au Ujerumani, kisha unaambiwa utapelekwa Saudia au Qatar.
Takriban kila Mkenya anajua kwamba mazingira ya kufanyia kazi katika mataifa ya Mashariki ya Kati ni sawa na ya enzi ya utumwa, haki za binadamu ni msamiati usiokuwepo, lakini Serikali ya Kenya iko radhi kuwatuma raia wake huko, yawakute ya kuwakuta!
Unaposoma makala hii, kuna visa vingi vya Wakenya kuuawa na kuteswa kwenye mataifa kadha ya Mashariki ya Kati kwa sababu waajiri wa huko wanaamini mfanyakazi asiye wa asili ya Kiarabu ni mtumwa anayefaa kudhulumiwa.
Hata lugha yao yenyewe haina neno la heshima la kumrejelea mfanyakazi wa nyumbani, anaitwa ‘mtumwa’. Na tatizo si lugha pekee, anatendewa kama mtumwa: anabakwa kwa raha zao, ananyonyesha mbwa, hana uhuru wa kutagusana na watu wengine nje ya nyumba anamofanya kazi, sikwambii vitambulisho vyake vinatwaliwa mara tu anapofika nchini humo.
Serikali haijawasaidia waathiriwa wa unyama unaoendelea huko, imeamua kuwafumbia jicho na kuwatuma wengine zaidi wakacheze kamari hatari na maisha yao.
Hilo linanisadikisha kwamba kuna manufaa fulani ambayo serikali inapata kwa kufufua na kuwezesha kufanyika kwa biashara ya utumwa.
Nashuku kwamba msukumo hapa ni tamaa ya pesa tu kama iliyotuingiza kwenye mkataba hatari wa kuwapeleka polisi wetu Haiti.
Serikali inataka kuvuna unono, angaa iokote ushuru hapa na pale, wala haijali kamwe kuhusu yatakayowafanyikia Wakenya watakaosajiliwa baada ya kuondoka Kenya.
Ikiwa hali si hiyo, kwa nini serikali imejiingiza katika shughuli ya kuwasajili watu wanaokwenda kufanya kazi nje?
Kikawaida, mawakala binafsi husajili watu wanaotaka kwenda kufanya kazi kwenye mataifa hayo bila kuihusisha.
Sasa inashirikiana kwa karibu sana na mawakala hao katika kufanikisha shughuli hiyo, lakini mazingira ya ukosefu wa uwazi na heshima kwa wanaotafuta kazi ni ule-ule ambao umekuwa ukiendelea tangu hapo.
Waliofanyiwa usaili na kukubalika wanaambiwa walipe Sh120,000 kila mmoja ili wapate kazi hizo kisha wajilipie nauli za ndege, takriban Sh80,000 kwenda Mashariki ya Kati. Hali imekuwa hii tangu mwanzo, kwa hivyo Serikali haiwasaidii kwa vyovyote.
Wengi, hasa wataalamu kama wauguzi, walichangamkia fursa hizo waliposikia kwamba serikali inahusika kwa kuwa walidhani hali ingekuwa tofauti, lakini wameishia kujuta na kutamauka.
Wanajiuliza serikali inawasaidiaje kwa kuwa shughuli yenyewe imegubikwa na siri kuu kama kaburi. Utamtoaje muuguzi mzima nchini bila kumwambia mwajiri wake ni nani, mshahara wake ni kiasi gani, na bado unamwambia ajilipie gharama za safari?
Watu si wajinga!
Kwa nini Serikali ya Kenya inashirikiana na mawakala wanaosifika kwa mateso chungu mbovu badala ya kushirikiana moja kwa moja na serikali za mataifa yanayohitaji wafanyakazi kufanikisha shughuli yenyewe?
Huu unakaa kama mchezo wa ‘taon’. Huenda hata mawakala hao ni Wakenya ambao wameona fursa ya kuitumia Serikali kujinufaisha.
Si siri kwamba baadhi ya maafisa wakuu wa Serikali ya Kenya wanamiliki kampuni za kuwasajili wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi.
Na kwa sababu ujanja wao unaishia Mashariki ya Kati, zile ahadi za kuwapeleka watu kwenye mataifa yaliyoendelea kama vile Australia, Ujerumani na Amerika hazizungumziwi tena.
Ikiwa Serikali ya Kenya ina nia safi katika mpango huu, kwa nini isishirikiane na mawakala wa mataifa hayo yaliyoendelea ilhali tunajua mengi hayawatozi hata ndururu wanaosajiliwa kwenda kufanya kazi huko?
Ninawajua wauguzi wengi ambao walisajiliwa na mawakala wa Amerika, wakalipiwa gharama zote na vipimo vya afya, nauli na waume au wake zao pamnoja na watoto wakapewa vibali vya kusafiria na kufanya kazi Amerika.
Kwa nini Serikali ya Kenya isishirikiane na mawalaka hao ambao hawahatarishi maisha ya raia wetu waliojasiria kujitafutia riziki nje ya nchi baada ya serikali hiyo-hiyo kushindwa kubuni fursa za kazi nchini?
Nawashauri Wakenya wanaotaka kwenda kufanya kazi nje ya nchi wajiepushe na mpango wowote ambapo Serikali inahusika, wanatozwa pesa, na wanakotumwa kufanya kazi ni Mashariki ya Kati.
Serikali ya Kenya imeshindwa kuwalinda wafanyakazi waliokutangulia kwenda huko, unadhani wewe una umuhimu gani kwake ndio ikulinde?
Usitapeliwe hali u macho.
Leave a Reply