Serikali kutumia wabunge kupigia debe SHA mashinani – Taifa Leo


SERIKALI inategemea Wabunge kusajili watu zaidi katika Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) na pia kutangaza mpango huo mpya.

Wabunge hao ambao kwa sasa wako kwenye likizo ndefu ya Krismasi hadi Februari mwaka ujao, wanatarajiwa kutumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi manufaa ya mpango huo mpya wa afya.

Katika mkutano usio rasmi wa hivi majuzi (kamkunji) uliohudhuriwa na Waziri wa Afya Deborah Mulongo, maspika wa mabunge yote mawili waliwasihi wabunge kuwahamisha wakazi kuhusu mfumo huo mpya.

Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula alisema kikao hicho kilikusudiwa kufafanua suala hilo ili wabunge katika mawasiliano yao wasichanganye umma zaidi.

‘Ninaamini kwamba kama viongozi, mnaweza kutumia afisi zenu kusaidia mchakato wa usajili wa wananchi ambao pengine hawajaambiwa kama usajili huo unagharimu pesa au la,’ Spika Wetang’ula alisema.

Spika wa Bunge la Seneti Amason Kingi alisema lengo la mkutano huo lilikuwa timu kutoka wizara kuwafahamisha wabunge ili wanapokwenda mashinani wawe na majibu ya maswali kuhusu mpango huo.

‘Kama viongozi, tuna jukumu la kuhakikisha ujumbe huu unafikishwa kwa watu inavyotakiwa,’ aliongeza.

Mbunge wa Mwala Vincent Musyoka alisema wamehimizwa kuhubiri injili ya SHA kwa watu.

“Kulikuwa na wito wa wazi kutoka kwa wizara na uongozi kuhubiri injili kwa watu wengi iwezekanavyo. Watu wanahitaji kuelewa aina na manufaa ya SHA kwa uwazi ikilinganishwa na NHIF,” Bw Musyoka alisema.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*