MRADI muhimu wa Rais William Ruto unaohusu nyumba za bei nafuu utakosa kwa umbali kutimiza malengo yake ya kujenga nyumba 200,000 kwa mwaka.
Waziri wa Ardhi, Alice Wahome, ambaye wizara yake inasimamia mradi huo, alisema nyumba zisizofikisha 1,000 ndizo zikabidhiwa wamiliki wake kufikia mwisho wa mwaka.
Alitaja changamoto kadhaa ikiwemo kesi za kortini na kucheleweshwa kwa fedha.
“Huenda nisiwe na nyumba 200,000 kwa mwaka jinsi tulivyoahidi lakini nina hakika nitakuwa na pengine nyumba 700 – 800. Shabaha yetu ni nyumba milioni moja katika muda wa miaka mitano. Tumeshindwa kufikisha idadi ya nyumba 200,000,” Bi Wahome alisema jana akihutubia vyombo vya habari, Nairobi.
Alisema mradi huo wa serikali ya Kenya Kwanza ulilemazwa baada ya kundi la wanaharakati na baadhi ya Wakenya kufika kortini kuupinga.
Mradi huo uliathirika zaidi kutokana na kucheleweshewa fedha katika bajeti ya 2022/2023.
Waziri, hata hivyo, alisema mradi huo umeshika kasi na akaelezea matumaini kuwa shabaha ya kujenga nyumba milioni moja katika muda wa miaka mitano sio jambo lisilowekana.
“Kulikuwepo ulegevu mwanzoni na kutatizwa na kesi za kortini. Kumekuwa na mambo chungunzima na nafikiri mbeleni, mradi huu haukuwa umepigwa msasa kuhusiana na ujenzi, mfumo wa ununuzi…kadri tunavyosonga mbele, huenda tukaokoa wakati uliopotea. Tuna takriban nyumba 140,000 zinazoendelea kujengwa na nyingine zaidi ya 600,000 ambazo zimeanza mchakato wa ununuzi,” alisema Waziri.
Bi Wahome alisema katika muda wa miezi miwili ijayo, nyumba 180 nchini kote zitakuwa tayari kukabidhiwa Wakenya , ikiwemo tano zilizopo vitongoji duni vya Mukuru.
“Tunatarajia kukabidhi umma nyumba hizo Machi. Kuna Vitengo vitano Mukuru tunajenga nyumba 13,000 Mukuru. Katika muda wa siku 60 zijazo tutakabidhi umma nyumba 1,080.”
Akitoa hotuba ya taifa Novemba mwaka jana, Rais Ruto alisema taifa linakabiliwa na upungufu wa nyumba ambapo angalau nyumba mpya 200,000 zinahitajika kila kwaka kwa miaka 10.
Katika bajeti inayotumika kwa sasa ya 2024/2025, Hazina ya Kitaifa ilitenga Sh32.5 bilioni kugharamia ujenzi wa nyumba za bei nafuu.
Aprili 2024, Tume ya Kutetea Haki za Kibinadamu (KHRC), na Katiba Institute ziliwasilisha kesi kupinga Sheria ya Nyumba za Bei Nafuu 2024 na kusimamisha serikali kuwakata Wakenya asilimia 1.5 na asilimia sawia kutoka kwa waajiri kugharamia mpango wa makazi.
Katika uamuzi uliotolewa Novemba 2023, korti iliafikiana na makundi ya wanaharakati na kutangaza sheria ya Nyumba za Bei Nafuu inakiuka katiba.
Hata hivyo, Februari 2024, wabunge walipitisha sheria nyingine ya Nyumba za Bei Nafuu 2024, iliyotiwa saini na Rais kuwa sheria 2024, hatua iliyowezesha utekelezaji wa ada hiyo na mradi huo kusonga mbele.
Leave a Reply