Serikali yasema imeweka mikakati Raila kushinda uenyekiti AUC – Taifa Leo


SERIKALI imetangaza kuwa imempanga Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga katika azma yake ya kuwania uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) huku kampeni zikiingia kipindi cha lala salama.

Katibu wa Masuala ya nchi za Kigeni Dkt Korir Sing’oei, ambaye pia ni mkuu wa sekretarieti ya kampeni ya Bw Odinga aliambia Taifa Leo kwamba, serikali na mgombeaji huyo wametimiza hatua zote zinazohitajika ili kushinda wadhifa huo wa bara.

“Tunaendelea vizuri. Kama unavyojua tumetembelea nchi zote tukiwa na ujumbe wa wazi wa kuungwa mkono na majibu yamekuwa ya kutia moyo. Tumeona rais, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na mgombeaji mwenyewe wamekuwa na ziara katika maeneo mbalimbali wakisaka kura,” Dkt Sing’oei alisema.

Aliendelea: ‘Tumefanya uzinduzi, mjadala na kufanya mahojiano na vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa na hatua muhimu sasa ni kupata uungwaji mkono kabla ya kupiga kura. Hii ni sehemu muhimu sana.”

Katibu alifichua kuwa Rais Ruto anatarajiwa kukutana na wakuu wengine wa nchi katika kampeni za mwisho huko Ghana alikoenda kuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa rais mpya.

“Rais atazungumza na wenzake na baadaye Mwezi huu atakuwa Afrika Kaskazini huku mgombeaji wetu akielekea Afrika Magharibi. Kwa ujumla tumejipanga,” aliongeza Dkt Sing’oei.

Rais Ruto wiki jana alimkaribisha Bw John Mahama nyumbani kwake Kilgoris katika Kaunti ya Narok kama sehemu ya kampeni za Kenya za kiti cha mwenyekiti wa Muungano wa Afrika.

Rais Ruto alijumuika na Bw Odinga katika mkutano huo.Mkutano huo ulijiri wiki moja tu baada ya rais kukutana na mwenyekiti wa AUC anayeondoka Moussa Faki Mahamat ambapo pia walijadili uchaguzi ujao wa bara.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*