UNAPOJIVINJARI msimu wa huu wa sikukuu kuwa mwangalifu usijihusishe na vituko vinavyoweza kukutia mashakani.
Ukiwa maeneo ya burudani epuka vitendo vinavyoweza kufanya usukumwe jela kama kupapasa au kugusa mtu sehemu za mwili unazofaa kufanya hivyo kwa idhini yake tena faraghani.
Hii ni kwa kuwa baadhi ya watu wakilewa huwa wanajisahau na kuanza kupapasa wengine kiholela.
Kisheria ni makosa kupapasa mtu bila hiari au idhini yake. Wengi wanaohusika na tabia hii ni wanaume hasa wanapolewa au wanapotembelewa na wapenzi wao.
Kulingana na sheria ya dhuluma za mapenzi ya Kenya ni makosa kumpapasa mtu au kumhusisha katika kitendo cha mapenzi bila idhini yake.
Kwa hivyo, kupapasa mtu bila idhini yake kwa kuwa ni mpenzi wako kunaweza kukutumbukiza mashakani.
Hata mtu akijiachilia au kukupata idhini umpapase, ni muhimu kuhakikisha kuwa ana umri wa zaidi ya miaka kumi na minane. Hii ni kwa wanaume na wanawake.
Kulingana na sheria, ni makosa kwa mwanamke kujihusisha kimapenzi na mvulana aliye na umri wa chini ya miaka kumi na minane sawa na ilivyo kosa kwa mwanamume kushiriki mapenzi na msichana ambaye hajafikisha umri wa miaka hiyo.
Ni muhimu kukumbuka kuwa kisheria, kabla ya kufikisha umri wa miaka kumi na minane, mtu huwa bado ni mtoto na analindwa na sheria za watoto.
Ni muhimu kuhakikisha umri wa mvulana na msichana kabla ya kuchukua hatua ya kujihusisha kimapenzi naye. Kuna watu ambao huwa na tabia ya kuishi na wapenzi wao katika nyumba zao msimu wa sherehe wakiburudishana.
Kwa wale walio na tabia hii au wanaopanga kufanya hivyo msimu huu, ningetaka kuwashauri wahakikishe kwamba hawafungii msichana au mvulana aliye na umri wa chini ya miaka kumi na minane kwa sababu wanaweza kukabiliwa na shtaka mbaya zaidi ya kuteka nyara na kuzuilia mtoto.
Kabla ya kutoka nyumbani, hakikisha umeacha watoto wako wakiwa na salama na kutunzwa vyema. Wazazi walio na tabia ya kuacha watoto wao bila mtu wa kuwatunza na kwenda kujivinjari kwa siku kadhaa vilabuni msimu wa sherehe pia huwa wanakosa na wanaweza kuadhibiwa wakifikishwa kortini.
Aidha, ni muhimu wamiliki wa vilabu na vyumba vya starehe na wafanyakazi wap kufuata sheria na kuepuka kuwauzia vileo pombe watu ambao hawajatimiza umri wa miaka 18.
Na sio kuwauzia pekee. Ni makosa kuruhusu watoto kuingia katika maeneo ya burudani na kunaweza kufanya mwenye biashara kupokonywa leseni na kutozwa faini.
Leave a Reply