Sheria:Vigezo vinavyoweza kufanya ‘njoo tuishi’ kutambuliwa kama ndoa – Taifa Leo


KUNA ndoa ambazo zinatambuliwa kwa kuchukuliwa kuwa zilifanyika hasa pale mwanamume na mwanamke wanapoishi pamoja kwa muda mrefu licha ya kutofunga mojawapo ya aina za zinazotambuliwa kisheria za kitamaduni, kikristo, kijamii, Kiislamu au Kihindu

Ndoa inaweza kuchukuliwa kuwa ilifanyika ikiwa mwanamume na mwanamke wanaishi pamoja kwa muda mrefu na kujionyesha kama mume na mke.  Hii yenyewe inaleta dhana kwamba wameoana  na inapopingwa, ni jukumu la wale wanaoipinga kuthibitisha kwamba kwa kweli hakukuwa na ndoa.

Ikiwa mwanamume na mwanamke wameishi pamoja kwa muda mrefu na katika mazingira ambayo wamepata sifa ya kuwa mwanamume na mke, uhusiano wao unaweza kuchukuliwa kuwa ndoa halali, ingawa kunaweza kukosa ushahidi chanya wa ndoa yoyote.

Ni ushahidi wenye nguvu na mzito unaoweza kufanya uhusiano kutochukuliwa kuwa ndoa. Ni muhimu kufahamu kuwa  uhusiano hauwezi kuchukuliwa kuwa ndoa iwapo mtu anaishi na mwingine aliye katika ndoa ya kikristo, kijamii na kihindu ambazo hazijavunjwa rasmi.

Hii ni kwa kuwa ndoa hizi huchukuliwa kuwa za mke mmoja na kwa hivyo ukiishi na mtu aliyetengana na mume au mke kabla yao kutalikiana, mtakuwa mumewekana kimada.

Kabla ya dhana ya ndoa kutokea, wahusika wanahitaji kuwa wameishi pamoja na kwa muda mrefu, na kuwa na vitendo vinavyoonyesha kwamba kuishi pamoja kwa muda mrefu si urafiki tu au kwamba mwanamke si kimada tu bali kuishi pamoja kwao kwa muda mrefu kunawasawiri kama wanandoa.

Kwa hivyo, isipokuwa mtu aweze kuthibitisha kwa nguvu kuwa uhusiano wa muda mrefu sio ndoa, mahakama kwa ujumla itachukulia ndoa ilifanyika iwapo tu wahusika walikuwa na uwezo wa kuoana inavyohitajika kisheria.U

Uwezo wa kuoana unafafanuliwa kama wahusika kuwa na zaidi ya miaka 18 walipoanza uhusiano wao,  kila mmoja wao awe alifanya hivyo kwa hiari, wawe na akili timamu na wasiwe katika makundi ambayo hayafai kuoana.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*