Shinikizo za maisha zilimwacha akining’inia padogo ila amegeuka msaada kwa wanaoumia kimya kimya – Taifa Leo


HUKU suala la afya ya akili likiendelea kupenya katika jamii ambayo miaka ya awali halikuchukulia kwa uzito, kijana Belden Magare ameibuka kuwa nembo ya ushindi licha ya giza nzito la mahangaiko.

Kama wanaume wengi nchini Kenya na kwingineko, alipambana na vita vya matatizo ya afya ya akili kimya kimya. Alizongwa na matatizo mengi ya kifamilia yaliyogeuka kuwa kesi kortini, na kuzidisha msononeko.

Ukosefu wa kazi nao ukaongeza mafadhaiko na kukata tamaa. Shinikizo kutoka kwa kanisa lake la kumtaka kuishi kulingana na matamanio ya jamii na dini zikamfanya ahisi kutengwa. Alihisi hakuna aliyeelewa mateso ya kisaikolojia aliyokuwa akipitia.

Kuanzia kushoto: Mbithe Mulinge, Mjumbe wa Kaunti ya Kitui, Belden Magare, Edwin Nyakundi, Msanii wa nyimbo za injili Winrose Mukabwa na Glantwil Ruvinzu, mkurugenzi wa elimu katika shirika la ‘Seed of Hope Foundation’ wakati wa uzinduzi wa shirika hilo. Picha|Leah Makena

“Katika kipindi hicho cha giza, nilielewa wazi unyanyapaa unaozunguka afya ya akili, haswa kwa wanaume.  Nilihitaji usaidizi wa afya ya akili ila hakuna aliyekuwa upande wangu na nikalazimika kupambana peke yangu,” anasimulia Belden.

Kana kwamba kutia chumvi kwenye kidonda, uhusiano wake, ambao ulikuwa chanzo cha faraja, ulivunjika wakati mchumba wake alipopata ujauzito wa mwanaume mwingine.

Usaliti huu ukamwingiza zaidi katika hali ya kukata tamaa na kumwacha akining’inia padogo.

“Afya yangu ya akili ilizorota hadi kufikia hatua ya kufikiria kujiua. Nilihisi mpweke, kwani nilitengwa na jamii ambayo mara nyingi hutarajia wanaume kubaki imara licha ya changamoto wanazopitia. Hata hivyo, katika nyakati hizo za giza, nilipata cheche matumaini, niliingiwa na hamu ya kuhakikisha kwamba hakuna mwanaume mwingine yeyote ambaye atateseka kimya kimya kama mimi,” anaeleza Beldene.

Alipata nafasi ya kuunda jukwaa ambapo wanaume wanaweza kutafuta msaada wa afya ya akili bila kuhofia kuhukumiwa. Hapo ndipo msingi wa Seed of Hope ulizaliwa.

Jeppy Collins, mbunifu wa maudhui akihudhuria hafla ya kuzinguliwa kwa shirika la Seed of Hope. Picha|Leah Makena

Tangu kuzinduliwa kwake Oktoba 2024, shughuli za shirika la Seed for Hope tayari zimeshika kasi na zaidi ya wanachama 25 wanafanya kazi pamoja kuleta mabadiliko. Misheni mbili  kuu za shirika la hili ni kutetea ufahamu wa afya ya akili miongoni mwa wanaume na kusaidia wanafunzi mahiri wasiojiweza ili waweze kuendeleza elimu yao.

“Kama sehemu ya dhamira yetu ya kuondoa unyanyapaa kuhusu afya ya akili miongoni mwa wanaume, shirika la Seed for Hope liliandaa mazungumzo ya Afya ya Akili na wanaume Desemba 8, 2024,” aliarifu Glantwill Ruvinzu, mkurugenzi wa elimu katika shirika la Seed of Hope Foundation.

Grantwil anasema kuwa shirika hilo linatafuta kikamilifu ushirikiano na makampuni, mashirika yasiyo ya serikali na watu binafsi wanaopenda afya ya akili na elimu.

Patric Obayi, Emmanuel Mwenda, Glantwill Ruvinzu na Morgan Adrian wakiwa kwenye hafla ya uzindui wa shirika la ‘Seed of Hope’. Picha|Leah Makena

“Ushirikiano ni ufunguo wa kupanua ufikiaji wetu na kuleta tofauti kubwa. Wale walio tayari kuunga mkono au kujiunga na programu zetu wanaweza kuwasiliana nasi. Kwa kufanya kazi pamoja, tunaweza kupanda mbegu za matumaini na kukuza jamii yenye afya bora,” anaeleza Ruvinzu.

Kulingana na Beldin, Seed for Hope Foundation inakua kwa kasi, ila anakiri kuwa wanahitaji usaidizi wa kujitolea, mshirika au hata wakili akisema kuwa mchango wa mtu yeyote utakuwa muhimu mno.

“Pamoja, tunaweza kuunda ulimwengu ambapo afya ya akili inapewa kipaumbele, na hakuna mtu anayepaswa kuteseka kimya kimya. Tuzime unyanyapaa. Afya ya akili ya wanaume ni muhimu,” anamalizia Beldine.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*