SHIRIKA moja lisilo la serikali sasa limekumbatia mpango ambapo linalenga kujenga kliniki kubwa ya kisasa ya kutibu ugonjwa wa yabisi (Arthritis) mashinani maeneo mbalimbali nchini.
Kliniki ya kwanza inaendelea kujengwa katika eneobunge la Likuyani Kaunti ya Kakamega ili kuwasaidia wanaougua maradhi hayo hasa mashinani, kupata tiba.
Shirika la Word Bicycle Relief limedhamini waendeshaji baiskeli 40 ambao walianza safari kutoka Mombasa hadi Busia wiki jana kama sehemu ya kuchangisha pesa za kusaidia kujenga kituo hicho.
“Pesa ambazo zimechangishwa kutokana na shughuli hii ya uendeshaji wa baiskeli zimesaidia katika ujenzi wa awamu ya kwanza ya kliniki hiyo kwenye ardhi ya ekari tisa.
“Hasa tunalenga kuhakikisha kuwa tunawasaidia wanaougua yabisi na pia kutoa hamasisho ya ugonjwa huo mashinani,” akasema Moses Ogola ambaye ni mratibu wa mpango huo.
Yabisi ni ugonjwa ambao umekuwa ukiwaathiri maelfu ya Wakenya na tiba yake huwa ni kibarua kupata hasa kwa Wakenya ambao wanaishi mashinani.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, kati ya dalili za ugonjwa huo ni maumivu, mwili kuwa mgumu, uvimbe ambao hulemaza mtu na kusababisha iwe vigumu kwake kutembea.
Kliniki inayojengwa Likuyani, itasaidia kwa kutoa matibabu na kuwaelimisha wagonjwa kuhusu njia ya kudhibiti yabisi na kuimarisha maisha yao.
Mkurugenzi Msimamizi wa kieneo wa World Bicycle Relief Maureen Kolenyo alisema kuwa shirika hilo limekuwa likishirikiana na wadau mbalimbali kushughulikia changamoto zinazoibuka za kiafya.
“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa wale ambao wapo mashinani wanafikiwa na mahitaji yao ya kimatibabu yanashughulikiwa,” akasema Bi Kolenyo.
Shirika hilo limejizolea umaarufu mkubwa kwa kuwapa wahudumu wa afya wa nyanjani baiskeli ili kuwasaidia kuwafikia na kuwahudumia wagonjwa.
Leave a Reply