Shirika laanika ‘uozo wa uongo na hongo’ wa utawala wa Rais Ruto – Taifa Leo


UTAWALA wa miaka miwili wa Rais William Ruto umepokea alama duni na shutuma kali kwa kukita mfumo wa ufisadi na kuepuka adhabu ili kujinusuru kisiasa.

Ripoti ya hivi punde zaidi ya shirika la Africa Centre for Open Governance (Africog) inaonyesha kuwa, Wakenya wengi wanaamini kuwa Kenya inaelekea pabaya chini ya serikali ya Dkt Ruto ya Kenya Kwanza.

Ripoti hiyo iliyotolewa Jumatatu, inatoa taswira mbaya ya hali ya taifa na kushutumu utawala wa sasa kwa kuwezesha mfumo mbovu unaowanufaisha wachache.

Ikifafanua tathmini yake mbaya, ripoti hiyo ilitaja kashfa kama vile mikataba ya mabilioni ya Adani iliyofutwa, sakata ya uagizaji wa mafuta ya kupikia, mchele na mbolea ya ruzuku kama baadhi ya sakata ambazo zimekuwa nembo ya utawala wa Kenya Kwanza.

Kuendeleza siasa za kujikinga kwa kuteua wapinzani

Ripoti hiyo inamshutumu Rais Ruto kwa kuendeleza siasa za kujikinga kupitia upendeleo, kandarasi za kutiliwa shaka na uteuzi.

Ripoti hiyo yenye kichwa ‘Mwelekeo Mbaya: Ufisadi nchini Kenya 2022-2024’, inaangazia utamaduni unaoendelea na kuongezeka kwa ufisadi nchini Kenya chini ya serikali ya Rais Ruto.

Mkurugenzi Mkuu wa Africog Gladwell Otieno alisema kuwa, ingawa Rais Ruto alifanya kampeni kwa ahadi ya kuunda Tume ya Kuchunguza Utekaji nyara na idara za Serikali,ametupilia mbali ahadi hiyo kimyakimya.

Badala yake, alisema, wasiwasi wa Dkt Ruto umekuwa kuokoa maisha yake ya kisiasa, ambao amekita mizizi katika utawala uliojengwa kwa hongo na ubarakala.

Kutokana na hali hiyo, ufisadi unaendelea kukithiri, kashfa zinaongezeka, ubadhirifu unaendelea, uozo wa taasisi umeongezeka na mfumo wa uchunguzi umemomonyoka.

Ripoti za ukaguzi za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu zimefichua matumizi mabaya ya fedha za umma katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, huku stakabadhi za mapato ya Sh15.5 bilioni kwenye tovuti ya malipo ya serikali ya e-Citizen zikikosa kuthibitishwa.

Mdhibiti wa Bajeti pia amefichua matumizi yasiyodhibitiwa kama tatizo kubwa la kitaifa.

Miradi katika afisi ya Rais

Sehemu kubwa ya matumizi huwa yanahusu miradi katika ofisi ya rais, wizara za Fedha, Usalama wa Ndani na ruzuku zinazoendeshwa na wizara kuhusiana na chakula na kawi.

Haya ni kando na matumizi ya kupita kiasi kwa manufaa ya kibinafsi ya viongozi wakuu wa utawala wa Rais Ruto.

“Anapokaribia mwisho wa mwaka wake wa pili akiwa rais, Wakenya wengi sasa wanaamini kuwa nchi inaelekea pabaya chini ya uongozi wa Ruto,” alisema Bi Otieno.

Mkuu huyo wa Africog alidai kuwa, siasa za upendeleo zinaendelea huku Rais akijaribu kuimarisha msingi wake wa kuungwa mkono kwa kuwazawadi wafuasi wake na kuwaalika wapinzani wake wa zamani serikalini.

Ripoti hiyo inadai Rais Ruto ameteua watu wanaochunguzwa kwa uhalifu katika baraza la mawaziri, huku serikali mpya ikijumuisha watu wapya katika nyadhifa kuu ambao walichaguliwa kwa uaminifu wao na kuzingatia maeneo wanayotoka badala ya sifa.

Bi Otieno alisema Rais Ruto ameteua wanasiasa wa chama chake cha kisiasa kushikilia nyadhifa nyingi serikalini ili kujipanga kwa uchaguzi mkuu ujao, lakini pia kutoacha nafasi ya ukosoaji.

Alisema kiongozi huyo alivutia vijana waliokuwa na matumaini kuelekea uchaguzi wa 2022 kwa ahadi ya kujenga uchumi kuanzia mashinani na kuondoa utawala wa familia zenye nguvu hadi kwa mahasla.

Ubadhirifu na matumizi mabaya ya pesa

Hata hivyo, ahadi hii ilififia haraka katika miaka miwili ya kwanza ya urais wake na hatimaye nafasi yake ikachukuliwa na rekodi ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma.

“Sasa, miaka miwili ya muhula wake, Ruto anaridhisha kundi dogo la washirika badala ya mahasla – vijana maskini, vijana ambao walijitokeza kumchagua kwa imani kwamba, rais mpya angeweka pesa mifukoni,” Bi Otieno alisema.

Alisema kuwa hatua ya Rais Ruto kuachana na ahadi yake ya maendeleo ya kiuchumi kumesababisha mojawapo ya changamoto kubwa nchini Kenya kwa rais – maandamano ya Gen Z.

Mkuu huyo wa Africog alisema kufikia mwisho wa 2023, asilimia 53 ya Wakenya waliamini kuwa nchi ilikuwa kwenye mkondo mbaya, na kufikia Septemba 2024, kura ya maoni ya Infotrak iliweka idadi hiyo kuwa asilimia 73.

Alisema Wakenya wamechukizwa sana na wanasiasa wao – ikiwa ni pamoja na upinzani – kiasi kwamba hawatarajii ufisadi kuangamizwa na mabadiliko katika serikali baada ya uchaguzi.

‘Rais si mgeni katika mfumo alioahidi kubadilisha’

Bi Otieno alisema kuwa rais si mgeni katika mfumo alioahidi kubadili na sasa anautumia vibaya, akimshtumu kwa kutumia mfumo wa sheria kama silaha kwa kufungulia na kuondoa mashtaka, kuunda miungano na uaminifu kupitia mamlaka ya afisi yake, na kuteua wafuasi kadhaa kushikilia ofisi kuu za umma kinyume na maoni ya umma.

Ripoti hiyo ilishutumu utawala wa Rais Ruto kwa kuhusika na kuondolewa kwa kesi mahakamani zinazokabili maafisa wakuu wanaoshtakiwa kwa makosa mbalimbali ya ufisadi na uhalifu wa kiuchumi na kuteuliwa kwao katika afisi kuu za umma.

Bi Otieno alitoa mfano wa kisa cha aliyekuwa mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Matibabu ya Kenya Davy Koech, ambaye alipokea msamaha wa rais mnamo Julai 2023 licha ya kupatikana na hatia mnamo 2021 na kuhukumiwa kifungo cha miaka sita gerezani.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*