Shirika lachimba mabwawa madogo 46 kuzima mafuriko Kisumu, Homa Bay – Taifa Leo


SHIRIKA moja linalohudumu mashinani limeanzisha mpango ambao utatoa suluhu ya kudumu kwa jamii maskini na wakazi wa kaunti za Homa Bay na Kisumu ambao wamekuwa wakitatizwa na mafuriko.

Shining Hope for Communities (SHOFCO) limechimba mabwawa madogo 46 ili kusaidia kupambana na mafuriko kwenye kaunti hizo mbili. Mabwawa hayo yapo kaunti ndogo za Seme, Nyando, Kisumu Magharibi, Muhoroni na Nyakach kwenye Kaunti ya Kisumu.

Katika Kaunti ya Homa Bay, mabwawa hayo yamechimbwa kaunti ndogo za Karachuonyo, Kabondo Kasipul na Kasipul.

“Mabwawa haya madogo yatasaidia kupunguza mafuriko, kulinda maisha, mimea na kudumisha miundomsingi,” akasema Mwanzishili na Afisa Mkuu Mtendaji wa Shofco Kennedy Odede.

Afisa huyo alikuwa akizungumza eneo la Awasi Kaunti ndogo ya Nyando. Mafuriko yamekuwa yakishuhudiwa sana Nyando, wakazi wakilazimika kuhama mara kwa mara na kuishi kwenye kambi ya muda.

Msaada wa Shofco unakuja wiki chache baada ya Mto Nyando kuvunja kingo zake na mji wa Ahero kufurika, nyumba na mashamba yakifunikwa na maji ya mafuriko.

Badala ya kutegemea serikali ya kitaifa na ile ya kaunti, Bw Odede alisisitiza kuwa ushirikiano wa wadau wote ndio utasaidia kumaliza mafuriko hayo.

“Lazima tuje pamoja kushughulikia suala hilo. Mabwawa haya madogo yatazuia uharibifu mkubwa ambao tumeushuhudia kwa muda mrefu,” akaongeza.

Mabwawa hayo madogo yamechimbwa katika nusu ekari ya ardhi na yanaweza kuhifadhi mita 200,000 za maji.

“Kando na kupunguza athari za mafuriko pia maji kwenye mabwawa haya yatakuwa yakitumiwa wakati wa ukame. Wakulima watayatumia mashambani, wakazi nyumbani na pia kuzima kiu cha mifugo,” akasema.

Bw Odede alisisitiza haja ya kukinga na kuyahifadhi maji ya mvua akisema ni kinaya kwa wakazi kulalamikia mafuriko kisha baadaye pia walalamikie ukame.

Mbunge wa Seme Dkt James Nyikal alimshukuru Bw Odede kwa kusaka suluhu kwa matatizo yanayozonga jamii.

“Uchimbaji wa mabwawa haya madogo yanasaidia siyo tu kupunguza mafuriko bali pia kupiga jeki jamii ijitegemee wakati huu wa mabadiliko ya tabia nchi,” akasema Dkt Nyikal.

Alisema mradi huo wa uchimbaji wa mabwawa unaonyesha kuwa wanajamii wakishirikiana basi wanaweza kupata angalau suluhu kwa matatizo yao badala ya kusubiri serikali iwawajibikie.

Bi Jennifer Atieno kutoka wadi ya Kabonyo Kanyagwal alishukuru Shofco akisema kuwa miradi mingine ambayo wameitekeleza imesaidia jamii hiyo.

“Sasa badala ya kulalamikia mafuriko tunaomba mvua inyeshe mabwawa yetu yajae maji,” akasema Bi Atieno.

Bw Odede alifafanua kuwa wanashirikisha umma kabla ya kuamua mahala pa uchimbaji wa mabwawa hayo na pia miradi mingine jinsi ambavyo imenakiliwa kwenye katiba.

Imetafsiriwa na CECIL ODONGO

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*