Shirika lataka Kindiki, Ichungwa, Kingi, Sudi wajiuzulu kwa ‘kuidhinisha utekaji nyara’ – Taifa Leo


SHIRIKA moja la kutetea haki za kibinadamu limewataka Naibu Rais Kithure Kindiki, Spika wa Seneti Amason Kingi, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Kimani Ichungwa, Mbunge wa Tiaty, William Kamket, Oscar Sudi (Kapsaret),John Waluke (Sirisia) na Waziri wa Masuala ya Ndani, Kipchumba Murkomen kujiuzulu likidai waliidhinisha utekaji nyara nchini.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Tume ya Haki za Kibinadamu  Kenya (KHRC) ilitaja matamshi  yaliyotolewa hadharani na viongozi waliotajwa hapo juu katika hafla tofauti nchini  likisema ni “uidhinishaji wa utekaji nyara kama jibu halali kwa madai ya ukiukaji wa sheria”.

KHRC ilisema kuwa matamshi ya viongozi hao yanaashiria uwezekano kwamba visa vilivyoendelea vya utekaji nyara vinavyoshuhudiwa nchini vinafadhiliwa na serikali. Shirika hilo  pia lilinukuu ujumbe wa Rais William Ruto wa Mwaka Mpya ambapo kiongozi wa nchi alikiri kwamba baadhi ya maafisa wa usalama wamehusika na vitendo visivyo vya kisheria.

“Maafisa wa usalama wa serikali wamekanusha hadharani kuhusika, huku Rais William Ruto akikiri kuhusika  kwao, akisema utawala wake utakomesha utekaji nyara,” lilisema.

Kundi hilo lilimkashifu Mbunge wa Kikuyu, Ichung’wah kwa kuunga mkono maoni ya Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu), Francis Atwoli, aliyedai kuwa watu waliotekwa nyara walikuwa wakijiteka nyara ili kujinufaisha kifedha.

Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah

“Katika kile kilichoonekana kuwa jaribio la kupotosha, Ichung’wah alitoa madai ya kushangaza kuhusu utekaji nyara na mauaji wakati wa uongozi wa   Rais Uhuru Kenyatta, akimshutumu Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya kwa kupanga njama iliyosababisha makumi ya watu kutoweka na miili  kutupwa katika Mto Yala,” shirika hilo lilisema.

Bw Ichung’wah na Atwoli walizungumza wakati wa mazishi ya mama ya Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula wiki jana.

Ni katika hafla hiyo hiyo ambapo Spika wa Seneti, Amason Kingi alisema serikali itatumia mbinu za kikatili kukabiliana na wakosoaji vijana huku akilaumu tabia zao kwa “ukosefu wa mwongozo wa wazazi.”

Mnamo Januari 3, alipokuwa akizungumza katika hafla moja huko Bungoma, Mbunge wa Sirisia, Waluke alisema kuwa utekaji nyara ni hadithi za kubuni ili kuchafua sifa ya Rais Ruto.

Siku mbili baadaye, wakati wa maombi ya madhehebu mbalimbali katika Elgeyo Marakwet, Bw Kamket alipuuzilia mbali wale wanaomtaka Ruto ajiuzulu akiwataja kuwa wavivu na kuonya kuwa wanaweza kuongeza muda wa Dkt Ruto.

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi. PICHA| MAKTABA

Mwenzake wa Kapsaret, Sudi hakuficha dharau yake kwa vijana wanaotumia picha za kejeli zinazozalishwa na AI kumkosoa rais na kusema kwamba ikiwa angekuwa Waziri wa Masuala ya Ndani, ingemchukua siku tatu tu “kushughulikia” wale wanaounda na kusambaza vibonzo vya rais.

Vitisho vya Bw Sudi vilijiri wiki moja baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani, Murkomen, mnamo Desemba 27 akiwa Bungoma, kukanusha kuwa kulikuwa na utekaji nyara na mauaji ya kikatili  chini ya utawala wa Rais Ruto.

“Kauli ya Murkomen inapuuza kunyongwa kwa vijana ambao wanatumia haki yao ya uhuru wa kujieleza dhidi ya utawala ambao umewaangusha vibaya,” KHRC ilisema.

Wanasiasa hao wote, Tume ilisema, wanaonekana kuiga Naibu Rais Kindiki, ambaye mnamo Septemba, alipokuwa akihudumu katika Wizara ya Masuala ya Ndani alifika mbele ya Kamati ya Usalama ya Bunge “ili halalishe matumizi ya nguvu kupita kiasi ya polisi dhidi ya waandamanaji  wasio na silaha”.

“Maoni ambayo wanasiasa hao walitoa yalikiuka katiba yetu. Maafisa wa serikali wanafungwa na maadili ya kitaifa na kanuni za utawala, ambazo ni pamoja na haki za binadamu, utawala wa sheria na demokrasia kama inavyopendekezwa katika Kifungu cha 10 cha katiba,” KHRC ilisema.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*