SHULE 11,000 za bweni kote nchini, ikiwemo vituo vya mafunzo ya kiufundi (TVET), zinatazamiwa kuanza kutumia mfumo wa gesi kupika chakula cha wanafunzi kufikia mwisho wa Juni 2025.
Akihutubu Jumatatu kwenye hafla ya kuzindua mpango wa matumizi ya gesi iliyoundwa kutokana na petroli iliyoyeyushwa – kwa Kimombo Liquefied Petroleum Gas (LPG) – iliyofanyika shule ya upili ya Jamhuri High School, Nairobi, Rais William Ruto alisema mpango huo ni sehemu ya sera ya serikali kuhamia matumizi ya nishati safi katika juhudi za kuhifadhi mazingira.
Rais alisema kufikia mwisho wa bajeti ya mwaka huu 2024-2025, shule za umma zitaanza kupika kwa kutumia gesi badala ya makaa au kuni, ambazo zinachangia pakubwa ukataji miti na athari za mabadiliko ya hali ya anga.
“Shule zote za umma na TVET zitapatiwa mitungi iliyojazwa gesi (LPG). Badala ya kutumia makaa sasa watakuwa wakitumia gesi. Shule zote sasa zitahama kutoka matumizi ya kuni na makaa na kuanza kutumia nishati safi,” alisema Rais Ruto.
Alifafanua kuwa mpango huo utakaoendeshwa katika taasisi zote za elimu za umma utapiga jeki azma ya kupanda miti 15 bilioni na kuongeza kiasi cha matumizi ya gesi nchini kwa jumla.
“Ili tutimize shabaha ya miti 15 bilioni, shule haziwezi kuendelea kukata miti,” alisema na kuongeza “mpango wetu ni kuongeza kiwango cha matumizi ya gesi kufikia kilogramu 15 kutoka kilogramu sita kwa kila mtu kila mwaka, na kuimarisha matumizi ya gesi kutoka asilimia 24 ilivyo sasa hadi asilimia 74 kufikia mwishoni mwa bajeti ya mwaka huu.”
Kando na kuhamia matumizi ya nishati safi, Dkt Ruto alisema mpango huo utaimarisha wanafunzi kiafya kwa kuwakinga kutokana na kuvuta hewa chafu ya kaboni inayotokana na matumizi ya kuni na makaa.
“Wanafunzi sasa hawatavuta hewa sumu ya kaboni. Watakuwa na afya njema,” akaeleza Rais.
Mpango huo utatekelezwa kupitia ushirikiano kati ya Wizara ya Kawi pamoja na sekta ya kibinafsi.
Huku akihimiza wadau katika sekta ya kibinafsi kujiunga na juhudi za serikali kwenye mchakato huo wa matumizi ya nishati safi, Rais alitangaza kuwa serikali itanunua gesi ya LPG kupitia Mfumo Wazi wa Zabuni ili kuhakikisha Wakenya wanapata gesi kwa bei nafuu.
Kuhusu wanafunzi wa Gredi 9, Dkt Ruto alisema madarasa yote 11,000 tayari yamekamilika na yapo tayari kwa wanafunzi shule zitakapofunguliwa Januari mwaka ujao.
Gavana Johnson Sakaja wa Nairobi na mawaziri Opiyo Wandati (Kawi) na Hassan Joho (Madini) ni miongoni mwa viongozi walioandamana na Rais katika hafla hiyo.
Leave a Reply