![Uhuru-Gachagua.jpg](https://informationcentre.co.ke/wp-content/uploads/2025/02/Uhuru-Gachagua.jpg)
HUKU mabadiliko ya kisiasa yakiongezeka kuelekea uchaguzi wa 2027, Mlima Kenya unageuka kuwa uwanja wa vita vya kulipiza kisasi kisiasa, wahusika wakuu wakiwania ubabe.
Mapambano haya yanazunguka Rais William Ruto, naibu wake Prof Kithure Kindiki, aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais Rigathi Gachagua, na aliyekuwa kiongozi wa Mungiki Maina Njenga.
Vichochezi vikuu vya hali hii ya kisiasa ni pamoja na mivutano ya mamlaka ndani ya utawala wa Kenya Kwanza, ahadi ambazo hazijatimizwa za uchaguzi, sera za ushuru, kuondolewa kwa Bw Gachagua, na kuibuka upya kwa Mungiki.
Seneta wa Murang’a Joe Nyutu anatoa muhtasari wa tatizo hilo kama wapiga kura wa Mlima Kenya kuhisi kusalitiwa.
“Tulimpa Rais Ruto asilimia 47 ya mamlaka yake kupitia kura zetu. Alichukua madaraka yetu na kuwapa wale waliotupinga katika Uchaguzi Mkuu wa 2022,” alisema.
Bw Nyutu anataja ahadi ambazo hazijatimizwa, ushuru mkubwa na kuondolewa kwa Gachagua serikalini kuwa sababu za kuongezeka kwa chuki.
“Mlima Kenya una kila haki ya kuhisi umealikwa kulipiza kisasi 2027 dhidi ya serikali na unataka kupiga kura kuiondoa,” akasema Bw Nyutu.
Ni mawazo ya aina hiyo ambayo yanaibua vita kati ya Ruto na Gachagua Mlimani. Bw Gachagua, kwa mujibu wa maoni ambayo amekuwa akitoa hadharani tangu Oktoba mwaka jana alipotimuliwa, anaonekana kuchochewa na ghadhabu dhidi ya mtu ambaye anasema alimfanyia kampeni Mlima Kenya 2022 lakini akamlipa kwa kumtimua. Naibu Rais huyo wa zamani ametangaza wazi kuwa nia yake ni kumfanya Dkt Ruto kuwa rais wa muhula mmoja.
![](https://informationcentre.co.ke/wp-content/uploads/2025/01/1736042883_191_maina-njenga-0101-2-300x180.jpg)
‘Ninakuahidi Bw Ruto kwamba hautafaulu katika Mlima Kenya. Hautafaulu kutugawanya ili ushinde. Hautafaulu kutushawishi turudi kwako. Sahau Mlima Kenya,’ Bw Gachagua alisema wiki mbili zilizopita akiwa kanisa moja katika Kaunti ya Laikipia.
Dkt Ruto, kwa upande wake, amepuuzilia mbali aliyekuwa naibu wake kama mtu anayezua mgawanyiko na asiye na jipya. Washirika wa Rais katika Mlima Kenya, wakiongozwa na Mbunge wa Mathira Eric wa Mumbi, pia wamemtaja Bw Gachagua kama ‘ mtu aliyeisha kisiasa ambaye hata hakuweza kujiendeleza kama naibu rais.’
Huku marafiki hao wawili waliogeuka kuwa maadui wakijaribu kukabana koo, mrengo mwingine wa kisasi dhidi ya Ruto na Gachagua unaonekana kuibuka kupitia aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta.
Hata baada ya Bw Kenyatta kukutana na Rais Ruto nyumbani kwake Ichaweri na taarifa kwa umma zilizofuata zikionyesha uwezekano wa wawili hao kuungana tena 2027, mambo yanaonekana kwenda kombo.
Hatua kuu ya hivi majuzi ya Bw Kenyatta ilikuwa kukosoa serikali na kuwahimiza vijana kutetea haki zao, lakini hakumtaja moja kwa moja Rais. Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Chama cha Jubilee Jeremiah Kioni anasema rais huyo mstaafu hawezi kuunga na Dkt Ruto.
‘Ruto alikuwa naibu wa Kenyatta kuanzia 2013 hadi 2022. Uhuru Kenyatta alijaribu kuwafahamisha Wakenya kwamba nchi haingekuwa salama mikononi mwa Ruto. Wakenya wamejua alikuwa sahihi. Ni nini kimebadilika kumfanya Kenyatta kumuunga mkono Ruto?’ alisema.
Kulingana na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta Charles Mwangi, tatizo kubwa ni kwamba ‘Bw Kenyatta anaonekana kulipiza kisasi dhidi ya Ruto na Gachagua’.
‘Ingawa Ruto anafanya kila awezalo kuurejesha Mlima Kenya, na Gachagua akijaribu kwa bidii kuunganisha eneo hilo kuelekea 2027, Bw Kenyatta anaonekana kuwa na mipango yake mwenyewe,’ Bw Mwangi alisema.
Aliendelea: ‘Inaonekana kweli kwamba Uhuru Kenyatta hajawasamehe Ruto na Gachagua kwa kumdhalilisha 2022 na njama ya kumbandua kama mfalme wa Mlima Kenya.’
![](https://informationcentre.co.ke/wp-content/uploads/2025/02/KINDIKI-KITHURE-300x180.jpg)
Bw Mwangi anataja matukio yaliyofuatia ushindi wa Muungano wa Kenya Kwanza ambapo mbuzi na kondoo wa familia ya Kenyatta waliibwa katika shamba lao la Northlands wakati wa maandamano ya upinzani mwaka wa 2023. Mnamo 2023, polisi walijaribu kuvamia nyumba ya mwanawe Kenyatta, Jomo, kwa kile walichodai kuwa umiliki wa bunduki. Pia kulikuwa na ripoti kwamba aliyekuwa mama wa taifa Mama Ngina ambaye ni mama wa Uhuru alipokonywa sehemu ya maafisa wake wa usalama.
‘Huenda ndiyo maana Ruto anatumia Naibu wake Kithure Kindiki na Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wa kurejesha Mlima Kenya, Gachagua anajaribu sana kuzuia hatua hiyo, Bw Kenyatta anaonekana kuunda mrengo mwingine,’ alisema Bw Mwangi.
Mbinu nyingine ya kulipiza kisasi inaonekana kugonganisha Mlima Kenya Mashariki na Mlima Kenya Magharibi katika muungano wa Gikuyu, Embu na Meru.
Kaunti za Embu, Meru na Tharaka Nithi (Mlima Kenya Mashariki) zinalengwa na washirika wa Dkt Ruto, wakiongozwa na Prof Kindiki, katika juhudi za kuzifanya kutengana na eneo la Kati (Mlima Kenya Magharibi) ambalo kwa sasa linaonekana kuwa nyuma ya Bw Gachagua.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply