TAKRIBAN wiki tatu tangu aondoke Old Trafford, Ruud van Nistelrooy amerejea uwanjani.
Mholanzi huyu ametangazwa meneja mpya wa Leicester baada ya siku 18 baada ya kukamilisha kazi ya kaimu kocha mkuu wa Manchester United.
Alipewa mikoba ya kuongoza the Foxes siku tano baada ya timu hiyo kumtimua Steve Cooper.
Tayari mashabiki wa Leicester City wameona anachoweza kufanya Ruud msimu huu.
Mechi mbili kati ya alizosimamia akiwa Old Trafford zilikuwa dhidi ya Leicester ambapo United iliibuka mshindi kwa 5 – 2 (Kombe la Carabao) na 3 – 0 katika ligi kuu ya Uingereza (EPL).
Kocha huyu mwenye umri wa miaka 48 aliongoza United tangu Erik ten Hag apigwe kalamu mwishoni mwa Oktoba na ujio wa kocha mpya Ruben Amorim mnamo Novemba 10.
Alijiunga na United katika wadhifa wa kocha msaidizi Julai kwa mkataba wa miaka miwili lakini hakupewa kazi ya kikosi cha kiufundi chini ya Amorim.
Sasa amerejea kazini kuongoza the Foxes ambao wako nafasi ya 16 kwenye jedwali la EPL.
Usimamizi wa Leicester City umemtimua Cooper ambaye ana tajiriba pana na kumchukua meneja ambaye hana tajiriba ya kiwango sawa kwani aliongoza katika kiwango cha juu alipokuwa kocha wa PSV kwa msimu mmoja tu ligi ya Uholanzi (Eridivisie).
Inaonekana huenda ni hatua ya kuweka timu hiyo katika hatari, lakini wanaomjua Van Nistelrooy wanasema ana msukumo, nia yenye nguvu na amejawa na shauku ya kufanya mambo kikamilifu.
Lejendari wa United
Manchester United walimnunua mshambulizi wa Uholanzi Van Nistelrooy kutoka PSV Eindhoven mnamo mwaka wa 2001 na alifunga mabao 150 katika mechi 219 kabla ya kuuzwa kwa Real Madrid 2006.
Aliyekuwa meneja wa United Rene Meulensteen anamkumbuka Van Nistelrooy kuwa mchezaji ambaye alikuwa na ari ya kushinda na wakati wote alitafuta mbinu ya kumbwaga mpinzani.
Akiwa Kocha, Van Nistelrooy bado ana shauku ya ufanisi kazini.
Alifanywa meneja wa akademia ya PSV baada ya kustaafu mwaka wa 2012 na akapandishwa daraja kuwa meneja wa timu ya kwanza 2022.
Baada ya kushinda kombe la Dutch Cup 2023, Van Nistelrooy alijiuzulu.
Katika msimu wake wa kwanza wa ligi ya Eredivisie, akaanza kutamaniwa na timu nyingine kwa wadhifa wa ukocha.
Hakuchukua ofa alizopewa, badala yake, alipumzika kwa mwaka mmoja kujifunza kutoka kwa kocha kutoka sehemu tofauti duniani – mabingwa wa Uhispania, Real Madrid na nyota wa Argentina, Boca Junior na River Plate.
“Katika matamanio ya kusafiri kuona michuano ya kandanda, alizuru kutazama mechi kubwa. Alizungumza na Martin Demichelis, meneja wa River Plate, kwa saa nyingi kuhusu ukocha,” akasema Marcel van der Kraan, mwandishi wa habari za michezo wa shirika la BBC.
Leicester City wanatarajiwa kunufaika kwa motisha yake ya kuimarisha wachezaji.
“Mtindo wake wa mchezo ni wa kiuhalisia kabisa usio na uoga,” alieleza Van der Kraan. “Siwezi kusema huwa anashambulia sana, lakini huonekana hatari.”
Licha ya kushinda mataji mawili na kufuzu kushiriki kipute cha Klabu Bingwa Ulaya, Van Nistelrooy alijiuzulu ikiwa imesalia mechi moja katika msimu wake wa kwanza PSV.
Van der Kraan anaeleza kuwa, wakati huo, uhusiano kati yake na wasaidizi ulikuwa umeharibika kwa sababu alitetea sana mitindo yake.
Vyombo vya habari viliripoti kuwa Van Nistelrooy alikuwa amekosana na wachezaji sita na wakamshtaki kwa bodi ya PSV.
Leave a Reply