Siku 180 msalabani kwa rais wa Korea Kusini aliyetumuliwa – Taifa Leo


RAIS Yoon Suk Yeol wa Korea Kusini ataishi roho mkononi kwa siku 180 zijazo kusubiri hatima ya Mahakama ya Kikatiba, kuidhinisha au kutupilia mbali uamuzi wa wabunge kupitisha hoja ya kumtimua mamlakani Jumamosi.

Jumla ya wabunge 204 waliunga mkono hoja ya kumbandua Yoon, baadhi yao wakiwa wa chama chake cha People Power Party (PPP).

Hoja hiyo ilifuatia jaribio la Yoon mnamo Desemba 3, 2024 kuanzisha sheria ya kijeshi, lililosababisha maandamano makubwa kote nchini humo.

Hata hivyo, uamuzi huo wa bunge utahitaji kuidhinishwa na Mahakama ya Kikatiba kabla Yoon kuvuliwa rasmi mamlaka ya kuongoza taifa hilo la bara Asia.

Wiki iliyopita juhudi za kumuondoa mamlakani Yoon lilifeli baada ya wabunge wa chama chake PPP kutohudhuria vikao vya bunge.

Raia wakiwa mbele ya bunge kushinikiza Rais Yoon Suk Yeol aondolewe mamlakani jijini Seoul, Juamamosi. PICHA | REUTERS

Jumamosi, mamia ya raia wanaopinga kiongozi huyo walifanya maandamano nje ya majengo ya Bunge la Kitaifa jijini Seoul, wakifurahia kupitishwa kwa hoja ya kumfuta kazi.

“Kwa raia wa Korea Kusini, tunataraji mtamaliza mwaka kwa furaha. Sherehe zote za kufunga mwaka zilizokuwa zimesimamishwa sasa zitarejeshwa,” akasema Spika Woo Wonshik wakati akitangaza rasmi matokeo ya kura kuhusu hoja ya kumtimua Yoo.

“Mustakabali wa Korea Kusini na matumaini yetu sasa yako mikononi mwetu. Matumaini yetu ni thabiti,” akaongeza Woo ambaye ni mwanachama wa chama kikuu cha upinzani Democratic Party.

Hoja ya kumtimua Yoon ilivutia uungwaji mkubwa wa umma huku matokeo ya kura ya maoni yakionyesha kuwa thuluthi tatu ya raia nchini humo walitaka atimuliwe mamlakani.

Raia walianza maandamano mara tu Yoon alipotangaza sheria ya kijeeshi mapema Desemba. PICHA | REUTERS

Baada ya uamuzi huo wa wabunge sasa hatima ya Yoon iko katika Mahakama ya Kikatiba ambayo ina siku 180 kuamua iwapo anapasa kuondolewa afisini au arejeshwe.

Ikiwa mahakama itaunga mkono hatua ya wabunge, uchaguzi wa rais mpya utaitishwa ndani ya siku 60 zijazo.

Yoon amesimamishwa kazi kwa muda baada ya kupitishwa kwa hoja ya kumtimua, na Waziri Mkuu Han Ducksoo ametwikwa wadhifa wa kuwa kaimu rais.

(Imeandaliwa na CHARLES WASONGA)



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*