Siku zako ndani ya ODM zinahesabika, Aladwa amchemkia Sifuna kwa kukosoa serikali – Taifa Leo


MBUNGE wa Makadara George Aladwa amesema kuwa siku za Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna katika chama hicho zimehasabiwa kutokana na hatua yake ya kuendelea kupinga serikali jumuishi na kile alichokitaja kama ‘kiburi’.

Bw Aladwa amemtaka Bw Sifuna ajiondoe chamani na ajiunge na mrengo wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua badala ya kupinga ODM ndani kwa ndani.

“Hapa ODM tumeamua kufanya kazi pamoja na serikali. Sifuna ni nani hata katika siasa za hapa Nairobi? Afadhali ajiondoe mapema kabla tumfikie kwa sababu hawezi kuwa katibu wa chama ilhali anapinga msimamo wa kufanya kazi na serikali tena anaongea kwa kiburi,” akasema Bw Aladwa kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Wikendi, Bw Sifuna aliashiria kuwa uhusiano wake na ODM unaelekea kusambaratika zaidi huku akionekana kuunga mkono azma ya Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka ya kuwania Urais mnamo 2027.

Wawili hao walihudhuria ibada ya kanisa Nairobi ambapo seneta huyo alisema haogopi kutimuliwa ODM kutokana na msimamo wake wa kupinga ushirikiano wa chama na Kenya Kwanza.

“Watu wengine wananiambia kuwa wamechoka kuwapigania Wakenya na kwamba hawakuzaliwa upinzani. Mimi nitaendelea kusema ukweli na wale ambao wamechoka kuwatetea Wakenya wahame ODM na wajiunge na UDA,” akasema.

“Mbona mjifanye mnampenda Rais ilhali yeye ni wa chama kingine?” akauliza huku akisisitiza chama hakitaachilia mtindo wake wa kuwatetea raia.

Bw Aladwa hata hivyo, anasema kuwa seneta huyo amevuka mipaka sasa na washampa ruhusa ya kuondoka ODM ashirikiane na Bw Musyoka au Bw Gachagua kwa sababu huko ndiko siasa zake za maasi zitavumiliwa.

“Bila ODM, Sifuna angepata wapi kura za useneta Nairobi? Hana kura hapa na mwelekeo ambao ameuchukua utamponza kisiasa 2027. Aondoke ODM la sivyo, tutamtoa,” akaongeza mwanasiasa huyo ambaye aliwahi kuhudumu kama meya wa Nairobi.

Majuma mawili yaliyopita wakati ambapo Rais William Ruto alihudhuria ibada katika eneobunge la Dagoretti, Nairobi, Bw Aladwa alimkaba koo seneta huyo akimshutumu kufika kwenye runinga ya kituo kimoja nchini kumdhalilisha Rais Ruto.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*