
MWALIMU wa shule moja ya Sekondari Msingi (JSS) iliyoko Nyamira aliyelazwa hospitalini baada ya kudaiwa kupigwa na mwalimu wake mkuu amekanusha madai kwamba alienda darasani akiwa mlevi.
Bw Vincent Onyancha, pia amedokeza kuwa yeye hunywa pombe tu wakati hayuko kazini na si mara nyingi kwa sababu ya ugumu wa maisha ambao haujamsaza kama Wakenya wengine wengi.
Mwalimu huyo wa eneobunge la Mugirango Kaskazini, amehoji kuwa pombe haijawahi kuathiri utendakazi wake kwa njia zozote zile.
Bw Onyancha anaeleza kuwa, mnamo wiki jana, Ijumaa Februari 21, 2025, alifika kazini akiwa amechelewa kidogo.
Alifululiza moja kwa moja hadi chumba cha walimu na kuchukua vitabu na vifaa vingine na kuelekea darasani tayari kwa somo na wanafunzi wake.
Kulingana na baba huyu wa mtoto mmoja, mara tu alipoanza kufundisha, mwalimu mkuu wa shule hiyo alijitosa darasani na kuanza kumwangushia makofi mazito mazito.
Mwalimu mkuu huyo alikuwa akimwuliza ni kwa nini alikuwa amefika darasani kuchelewa.

“Nilikuwa nimefika tu darasani na nimekwisha tulia alipoingia kwa nguvu. Aliniuliza kwa nini nilichelewa kufika shuleni. Kabla hata sijatoa maelezo, alinishukia kwa mateke na makofi. Alinivuta nje ya darasa huku wanafunzi wangu wakitazama kwa mshangao,” Bw Onyancha alidai.
Aidha, Bw Onyancha alidai kuwa mkuu huyo wa shule alizidi kumdhulumu alipompeleka ofisini kwake.
“Alinipiga bila huruma. Aliniangusha sakafuni katika afisi yake na kunikanyaga mgongoni. Nilijaribu kujieleza lakini hakusikia lolote. Sikuaibika tu mbele ya wanafunzi wangu bali pia machoni pa walimu wenzangu,” Bw Onyancha alisema.
Taifa Leo ilikutana na Bw Onyancha Jumanne asubuhi alipokuwa akitoka katika hospitali ya kibinafsi katika Mji wa Ikonge, ambako alikuwa amelazwa.
Wasimamizi katika Hospitali ya Medstops walikataa kufichua kiwango cha majeraha ambayo mwalimu huyo alikuwa amepata, wakidai kuwa kufanya hivyo kunaweza kuweka kituo hicho katika hali mbaya.
“Sitaki kuzungumzia sana suala hili kwa sababu linachunguzwa na asasi nyingi. Kuna mengi yanazungumzwa kuhusu mwalimu huyo na kwa hivyo, tungependa kutozungumza zaidi,” msimamizi wa kituo hicho ambaye alikataa kutaja jina lake alisema.
Juhudi za Taifa Leo kupata maoni kutoka kwa mwalimu mkuu anayetuhumiwa hazikuzaa matunda kwani walinzi wa shule hiyo walituzuia kuingia shuleni.
“Sitawaruhusu kuingia wala kuwapa nambari zake za simu. Nina maagizo makali ya kutoruhusu wanahabari kuingia kwa sasa,” mlinzi mmoja kwenye lango la shule hiyo alijibu.
Bw Onyancha aliajiriwa mwaka wa 2023 na akawekwa katika shule hiyo kama mwalimu wa JSS baada ya kusaka kazi kwa zaidi ya miaka mitano.
Kufuatia masaibu yake, Bw Onyancha ameitaka Tume ya Huduma na Uajiri wa Walimu (TSC) na mamlaka zote husika kuchunguza kesi yake kwa kasi na kuchukua hatua zinazofaa.
“Ninaomba TSC na wote wanaohusika kuchunguza tukio hili kwa haraka ili haki itendeke ninapotarajia kurejea kazini,” Bw Onyancha alisema.
Leave a Reply