Tahadhari kuhusu ulaji wa nyama msimu wa sherehe – Taifa Leo


BODI ya Madaktari wa Mifugo nchini (KVB), imewataka Wakenya kuwa waangalifu wanapokula nyama msimu huu wa sherehe.

Ikihutubia wanahabari mnamo Jumatatu, Desemba 23, bodi ilitoa wito kwa Wakenya kununua nyama kutoka kwa maduka yaliyoidhinishwa nchini pekee.

Wakenya walitahadharishwa haswa dhidi ya kula nyama kutoka kwa wanyama waliokufa, ambayo madaktari wa mifugo wanasema kuwa inauzwa kwa wanunuzi wasio na habari kwa bei ya chini.

Umma ulihimizwa kununua nyama iliyokusudiwa kwa matumizi ya binadamu pekee kutoka kwa maduka yanayouza nyama yenye stampu za kuiidhinisha za wataalamu wa serikali.

“Tumekuwa tukiona watu wakichinja wanyama kwa nyama ya matumizi ya nyumbani lakini ninakumbusha kila Mkenya kwamba afya yako inaanza na wewe,” ilisema bodi ya madaktari wa mifugo.

“Unafaa kununu nyama ambayo imeidhinishwa na ambayo ina stampu ambayo huwekwa na afisa aliyeidhinishwa,” iliongeza.

Wakenya walishauriwa pia kuwataka wachinjaji kuonyesha cheti cha kuidhinishwa kusafirisha nyama kutoka kichinjioni hadi dukani.

Onyo la KVB lilijiri baada ya Wizara ya Afya kuwaonya Wakenya kuepuka kula nyama ambayo haijakaguliwa na maafisa walioidhinishwa au kutoka kwa wanyama waliokufa.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari Jumatatu asubuhi, Katibu wa Afya Mary Muthoni aliwashauri Wakenya kutumia vyakula vilivyopikwa vyema ili kuzuia kuambukizwa na kutumia maji safi, yaliyotibiwa au kuchemsha kupikia na kunywa.

“Ili kudumisha usalama wa chakula na usafi, ni muhimu kuzingatia usafi kamili wakati wa kuandaa mlo. Nawa mikono mara kwa mara kwa sabuni na maji yanayotiririka, na uhakikishe kuwa vyakula vyote vimepikwa vizuri,” katibu Muthoni alisema.

Ili kuzuia kuenea kwa magonjwa, Wakenya walihimizwa kujikinga na hali mbaya ya hewa. “Funika mdomo na pua wakati wa kukohoa au kupiga chafya, na kuvaa barakoa katika maeneo yenye watu wengi,” alishauri Katibu Muthoni



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*