MSIMU wa sherehe za Desemba na Mwaka Mpya umefika na kuleta msisimko, watu wakisafiri kwenda maeneo mbalimbali kwa starehe.
Hata hivyo, kadri msimu wa sikukuu unavyozidi, ndivyo uwezekano wa ajali za barabarani unavyoongezeka.
Mnamo 2023, zaidi ya watu 300 walikufa msimu wa sikukuu kati ya Desemba na Mwaka Mpya. Magari ya uchukuzi wa umma (PSVs), ambayo yanajulikana kwa kubeba abiria kupita kiasi na mwendo kasi wa juu kipindi hiki, ili kuongeza faida ni miongoni mwa yaliyohusika katika ajali.
Takwimu kutoka kwa Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) na polisi wa trafiki zinaonyesha kuwa idadi ya vifo huongezeka mnamo Desemba katika maeneo ambayo yametambuliwa kuwa hatari kwa ajali za barabarani.
Kulingana na NTSA, waliofariki katika ajali za barabarani waliongezeka kutoka 20,191 mwaka wa 2023 hadi 21,620 kufikia Novemba 30, 2024.
Ukanda wa Bonde la Ufa ndio wnye maeneo mengi hatari kwa ajali nchini ukiwa na maeneo 13 yaliyotambuliwa kuwa hatari, huku Kaskazini Mashariki na Mashariki yakiwa na maeneo machache zaidi.
Mengi ya maeneo hatari yanapatikana katika barabara ya Nairobi-Nakuru-Eldoret, inayounganisha Kenya na Uganda, Sudan Kusini, Rwanda na Burundi.
Barabara kuu hiyo, iliyopewa jina la utani la kutisha “Barabara Kuu ya Kuzimu,” imekuwa na vifo 42 tangu Januari 2024. Maeneo mengine hatari kwa ajali ni Karai karibu na mji wa Naivasha ambapo watu 40 waliangamia mwaka wa 2017, na Kinungi-Naivasha, Gilgil-Kikopey, na St Mary’s Mbaruk.
Eneo lingine lenye sifa mbaya ni sehemu ya Salgaa, inayoanzia Daraja la Ngata hadi Sachangwan. Mnamo Agosti 20,2024 mwaka huu, watu 13 walifariki katika eneo la Salgaa kwenye barabara kuu ya Nakuru-Eldoret.
Maeneo mengine katika kusini mwa bonde la ufa ni Mau Summit – Londiani, Timboroa-Makutano, na vilima vya Pinyiny kwenye barabara ya Narok-Maai Mahiu. Barabara ya Bomet -Narok pekee imesababisha zaidi ya vifo 15 tangu mwaka uanze.
Jijini Nairobi, barabara kuu ya Thika yenye urefu wa kilomita 50 imeorodheshwa kuwa mojawapo ya barabara hatari zaidi, ikirekodi vifo 13 kati ya Januari na Aprili 2024.
Barabara ya Outering na Barabara ya Kangundo zinafuata kwa karibu, kila moja ikiwa na watu 12 waliofariki katika ajali hasa watembea kwa miguu wakivuka barabara bila kutumia daraja.
Takwimu zilizonaswa na NTSA kati ya Januari 1 na Aprili 30, 2024, zinaonyesha kuwa Nairobi ilirekodi vifo 176 kutokana na ajali za barabarani, kati ya 1,554 kote nchini, huku barabara kuu ya Thika pekee, ikigharimu maisha ya watu 13.
Data ya NTSA 2024 iliorodhesha barabara ya Waiyaki katika nafasi ya tatu kwa zile hatari zaidi, ikisababisha vifo vya watu 10 katika kipindi kinachokaguliwa.
Barabara za Eastern bypass, Juja, na Ngong zimeshika nafasi ya nne, huku ripoti ikionyesha watu saba waliangamia barabarani kwa muda huo huo.
Barabara nyingine kuu za Nairobi ni Kangundo Road, Northern Bypass, na Jogoo Road.
Katika eneo la Mlima Kenya, Daraja la Nithi kwenye barabara ya Meru-Embu ndilo eneo hatari zaidi kujengwa kwake mwaka wa 1985.
Maeneo mengine hatari kwa ajali katika eneo hili ni pamoja na Kiganjo- kwenye Barabara ya Nyeri-Narumoru na sehemu ya Limuru-Uplands.
Thika Blue Post kwenye Barabara ya Sagana Bridge, kwenye barabara kuu ya Nyeri – Nairobi, sehemu ya Kianugu kwenye Barabara ya Nyahururu na Barabara ya Kiambu – Muthaiga ni baadhi ya barabara kuu katika eneo hili ambazo ni hatari kwa ajali.
Maeneo mengine ni Makutano- Kutus kwenye barabara ya Makutano-Embu na eneo la Makongeni kwenye barabara ya Thika-Garissa.
Katika eneo la Nyanza, maeneo maarufu kama vile Awasi kwenye barabara kuu ya Kisumu-Kericho, Kiboswa kwenye barabara ya Kisumu-Kakamega, na Daraja Mbili huko Kisii yanaendelea kuwa hatari kwa ajali.
Maeneo hatari katika ukanda wa Magharibi ni pamoja na Kaburengu, Daraja la Yala, na Chavakali kwenye barabara ya Kakamega-Chavakali, ambayo hivi majuzi lori la mafuta lilianguka na kuua watu 10 mnamo Novemba 15, 2024.
Pwani, maeneo ambayo ni hatari ni Mombasa Nairobi hasa Maungu-Voi, Mazeras-Miritini, na barabara kuu ya Mombasa-Nairobi, kama vile Chumvi, Salama – Sehemu ya Sultan Hamud kuteremka Mlima Kiu, Mtito hadi Mto Tsavo.
Kwa mujibu wa NTSA eneo la Jiwe Tanga, Malindi, Waa kwenye makutano ya Kwale -Matuga na Makutano ya Navy (mzunguko wa Mtongwe) kando ya barabara ya Lunga Lunga –Likoni ni hatari kwa ajali.
Maeneo hatari kwa usafiri ukanda wa Mashariki mwa Kenya ni Machakos – Sehemu ya Barabara ya Wamunyu, Kithangathini huko Machakos, barabara ya Wamunyu, Mlololongo-Njia ya Klabu Ndogo ya Dunia – Namanga na daraja la Mto wa Mawe.
Leave a Reply