WASHINGTON, AMERIKA
RAIS mteule Donald Trump ameshutumu Ukraine kwa kutumia makombora makali iliyopewa na Amerika kuvamia Urusi, kauli ambayo inaashiria huenda akabadilisha sera za nchi hiyo dhidi ya Ukraine.
Trump alishutumu kitendo hicho akisema kinachochea tu kuendeleza vita hivyo vikali wakati ambapo juhudi zinastahili kuelekezwa katika kupata amani.
“Kinachoendelea ni kibaya sana na hakifai kuruhusiwa kabisa. Sikubaliani na hatua ya makombora kurushwa Urusi,” akasema.
Trump mnamo Alhamisi alitajwa Mtu maarufu zaidi wa 2024 na Jarida la Times Magazine.
Rais Joe Biden mwezi uliopita aliondoa marufuku ya Amerika yaliyozuia Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu dhidi ya Urusi.
Hii ilifasiriwa kama juhudi zake za mwisho za kusaidia Ukraine kufanikiwa kwenye vita dhidi ya Urusi kabla ya kuondoka mamlakani mnamo Januari.
Alichukua hatua hiyo baada ya kilio cha Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy kuwa walihitaji kutumia silaha hizo dhidi ya Urusi.
Ikulu ya White House ilisema ilichukua hatua hiyo baada ya wanajeshi 15,000 kutoka Korea Kaskazini kuungana na Urusi kwenye vita hivyo na kutumwa kwenye mpaka wa Ukraine.
Trump amenukuliwa wakati wa kampeni akisema nia yake ni kumaliza vita hivyo ambavyo vimedumu kwa muda wa miaka mitatu.
Hata hivyo, hakutoa ufafanuzi wowote jinsi ambavyo atatekeleza mpango huo japo akakiri kuwa kujiunga na majeshi ya Korea Kaskazini kwenye vita hivyo kunadidimiza zaidi matumaini ya kupatikana kwa amani.
“Nataka amani na njia pekee ya kuhakikisha kuna amani ni pande zote kusitisha vita,” akasema Rais Trump.
Trump atakuwa akichukua usukani mnamo Januari 20 na wikendi iliyopita, alikutana na Zelenskiy na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron jijini Paris.
Kauli ya Trump kuwa atamaliza vita hivyo hata hivyo imezua shauku kuwa atafanya hivyo kwa kuzingatia matakwa ya Urusi.
Duru zinaarifu kuwa Zelenskiy alimtaka Rais Trump kuhakikisha Ukraine usalama wake iwapo kutakuwa na muafaka wowote unaoshirikisha Urusi.
Trump alisikitika kuwa idadi ya watu ambao wamekufa kwenye mgogoro huo hasa mwezi uliopita ni wengi na vita hivyo vinastahili kukomeshwa.
“Nazungumza na pande zote mbili na makubaliano yatakuwa mazuri kwa pande zote,” akasema.
Alipoulizwa iwapo atakatiza msaada wa kibinadamu na kijeshi kwa Ukraine, Trump alinywea na kusema hawezi kufichua mpango wake kwa sasa kwa sababu huenda ukaibua hisia mbalimbali.
Pia alikataa kufichua iwapo amezungumza na Rais wa Urusi Vladimir Putin tangu ashinde uchaguzi. Vita kati ya Ukraine na Urusi vimeingia hatua ambayo baadhi ya mataifa ya Magharibi yamesema ni hatari sana.
Mnamo Novemba 21 Urusi ilirusha kombara yake mpya na hatari zaidi inayofahamika kama Oreshnik katika mji wa Dnipro Ukraine.
Leave a Reply